Featured Kitaifa

SERIKALI KUJENGA VYUO VITATU VYA WENYE ULEMAVU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na waandishi wa habari mjini Kasulu leo Agosti 3, 2022, kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2021/22 na Mwelekeo wa Bajeti ya Mwaka 2022/23 mjini Kasulu, Kigoma.

Na: Mwandishi Wetu – Kasulu, Kigoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuwawezesha Watu wenye Ulemavu kwa kujenga vyuo vipya vitatu vya ufundi stadi na kuvifanyia marekebisho vituo vinne ili wawe na uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kasulu leo Agosti 3, 2022, kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya ofisi hiyo kwa Mwaka 2021/22 na Mwelekeo wa Bajeti ya Mwaka 2022/23. Waziri Ndalichako alisema kuwa serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuleta ustawi wa kiuchumi kwa Watu wenye Ulemavu.

Masuala mengine ambayo bajeti hiyo itatekeleza ni pamoja na. Kufanya kaguzi 4,800 katika maeneo ya kazi pamoja na Kuratibu na kusimamia upangaji wa Kima cha Chini Mshahara katika Sekta Binafsi.

Aidha, alieleza kuwa Ofisi hiyo itaratibu suala la Kupunguzwa kwa kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa Sekta Binafsi kutoka asilimia 0.6 hadi kufikia asilimia 0.5 hivyo kuweka uwiano sawa katika uchangiaji baina ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma.

Mhe. Ndalichako ametaja vipaumbele vingine kuwa ni; Kuratibu mafunzo ya Ujasiriamali, kwa makundi maalum ya vijana (Mama wadogo, Vijana (WAVIU) katika mikoa 6 pamoja na Kutoa Mikopo kwa vikundi vya vijana vilivyokidhi vigezo kwa mujibu wa Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Aidha, kiasi cha Shilingi 1,000,000,000 kimetengwa kupitia ofisi hiyo.

Aliongeza kuwa, Serikali itatoa mafunzo kwa vijana 500 juu ya ujuzi wa uchumi wa blue kupitia ufugaji wa Samaki kwa njia ya vizimba; Uchumi wa Bluu una fursa nyingi hivyo Serikali inalenga kutoa Mafunzo haya ili kuwawezesha Vijana kunufaika na fursa hizo.

“Tutajenga Vituo 5 atamizi kwa vijana wanaopata Mafunzo ya uanagenzi, lengo la Vituo hivyo ni kutoa fursa kwa Vijana, kukuza na kuendeleza Ujuzi wao, aidha, Vituo hivyo vitatoa fursa kwa Vijana Wajasiriamali kuongeza Bidhaa zao thamani ili zifikie kiwango cha kuingia sokoni,” alisema

Katika hatua, nyingine  Mhe. Ndalichako amewashukuru wadau wa UTATU (Serikali, Vyama vya Wafanyakazi, na Waajiri) kwa kutekeleza kwa Sheria za Kazi nchini. Aidha, amewapongeza watumishi wa yake  kwa utekelezaji mzuri wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 na amewataka kuendelea kufanya kazi kwa ari, juhudi, ubunifu na kujituma  na kutanguliza uzalendo mbele.

About the author

mzalendoeditor