Featured Kitaifa

DC SHEKIMWERI AONYA UPOTOSHAJI ZOEZI LA SENSA

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna-DODOMA

MKUU wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23,mwaka huu linalenga kulisaidia Taifa kupata takwimu sahihi za kupanga maendeleo hivyo kuwataka wananchi kujiepusha na kuwapuuza watu wanaopotosha zoezi hilo kuwa lina madhara.

Akizungumza na mzalendo blog Agosti 3,2022,Jijini Dodoma amesema kuna kila sababu ya wana Dodoma kushiriki ipasavyo kwenye sensa hiyo ili waendelee kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Tunapaswa kujiuliza hii ni mara ya kwanza sensa kufanyika?je kuna ambao walipata madhara baada ya kuhesabiwa?sensa zote zilizopita hakuna mtu aliyejitokeza hadharani kwamba amepata madhara,tujiepushe na wapotoshaji, tuwabeze, tuwapuuze na tusiwafuate,”amesema.

Ametaja kazi nzuri anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan katika Jiji hilo ikiwemo ujenzi wa barabara za mzunguko,barabara za katikati ya Jiji,mji serikali,uwanja wa ndege wa Msalato na kiwanda cha mbolea cha Intracom ambapo ili kutekeleza hayo ni lazima kupatikana takwimu za watu.

“Tunaona Sh.Bilioni 12 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanawake,vijana na wenye ulemavu,Sh Bilioni 9.4 kwa ajili ya ujenzi wa soko la wazi la Machinga,hii ni heshima kubwa ambayo Rais ameionyesha katika jiji la Dodoma,hivyo najitokeza hadharani kuwaomba wakazi wa Dodoma Agosti 23,mwaka huu tuhesabiwe sisi na familia zetu,”ameongeza.

Zoezi la sensa ya watu na makazi ina umuhimu mkubwa katika nchi ikiwemo kuisaidia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa dira ya maendeleo yam waka 2025,na inasaidia kujua ongezeko la idadi ya watu ili kurahisisha kupanga maendeleo.

About the author

mzalendoeditor