Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, mkoani Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaoshirki katika Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kufungua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaoshiriki katika Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kufungua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax (wa pili kulia) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Meja General Ibrahim Mhona (kushoto) baada ya kufungua Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022. Wa pili kushoto ni Kansela wa Chuo cha Ulinzi Tanzania, Balozi Matern Lumbanga.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka washiriki wa kozi fupi ya 13 ya viongozi watambue, wafuate na waisimamie falsafa ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iliyojielekeza katika kuwahudumia watanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kuona mabadiliko ya kimtazamo, ushauri na maamuzi watakayoyafanya yanapaswa kuakisi walichokipata kupitia kozi hiyo mara baada ya viongozi hao kurudi kwenye maeneo yao ya utendaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 2, 2022) alipofungua kozi fupi ya 13 ya viongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Dar Es Salaam. Pia kozi hiyo itawaongezea uelewa na ufanisi katika eneo zima la ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kwamba washiriki wote, watatumia kikamilifu fursa hiyo adhimu kushiriki kwa umakini na uhodari wa hali ya juu ili kuongeza uelewa wao wa masuala mtambuka hususan ya kiulinzi, kiusalama na kistratejia.
Kozi hiyo inahudhuriwa na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Waandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi za Kimkakati za Serikali.
“Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu mafunzo haya mtakuwa mmebadilika kimtazamo na hilo halinabudi kujidhihirisha kwa Wizara na Taasisi mnazotoka kuzungumza lugha moja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu.”
“Kwa kufanya hivyo, mtasaidia sana kusukuma maendeleo ya nchi yetu kwa haraka hasa katika kipindi hiki ambapo Serikali inalenga kukuza uchumi wa viwanda. Sambamba na hilo, tunapaswa kutambua kwamba changamoto za sasa ni mtambuka na si rahisi kutatuliwa na Wizara au Taasisi moja moja.”
Akizungumzia Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa chuo hicho uhakikishe kozi hiyo inakuwa endelevu ili viongozi wengi zaidi wapite hapo na kufunzwa masuala muhimu yanayohusu ulinzi na usalama kwa nchi yetu.
“Tunahitaji viongozi, watendaji wakuu na maafisa waandamizi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na ofisi za kimkakati watambue na kuzingatia maslahi ya nchi, uzalendo, tunu zetu na nidhamu ya kazi kwenye utendeji wao.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema chuo hicho tangu kianzishwe Septemba 2012 kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kutoa kozi ndefu 10 pamoja na kozi fupi 12.
Mkuu huyo wa chuo ameongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kujitangaza na kukubalika kimataifa ambapo viongozi kutoka mataifa 16 wamehudhuria kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo.
Naye, Kansela wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Balozi Dkt. Marten Lumbanga amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa viongozi yataleta matokeo chanya kwa washiriki na kulifanya Taifa lisonge mbele na salama kwani wataongezewa ueleewa na umakini katika usimamizi madhubuti wa sera kwa usalama wa nchi.