Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO ASHIRIKI IBADA KIJIJINI KASUMO MKOANI KIGOMA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakishiriki Ibada ya kawaida ya Asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022 baada ya kumaliza kushiriki Ibada ya kawaida ya asubuhi Kijiji hapo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakiongozana  na Paroko wa Parokia ya Kasumo Padre Joseph Mashaka (wa pili kushoto) pamoja na Padre Francis Laswai ( wa Kwanza kushoto) mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya kawaida ya Asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma leo tarehe 29 Julai 2022.

******************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiambatana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wameungana na waumini wa Kijiji cha kasumo mkoani Kigoma katika kushiriki Ibada ya kawaida  ya katikati ya wiki katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani iliopo Kijiji hapo. Ibada hiyo imefanyika leo tarehe 29 Julai 2022 na kuongozwa  na Paroko wa Parokia hiyo Padre Joseph Mashaka akishirikiana na Padre Francis Laswai.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Padre Francis Laswai ameiomba serikali kuusaidia mkoa wa Kigoma katika sekta ya kilimo ili waweze kuzalisha mazao mengi zaidi kutokana na uwepo wa mvua za kutosha katika mkoa huo. Padre Laswai ameongeza kwamba mkoa huo unahitaji kilimo cha kisasa hivyo wataalamu wa kilimo wenye uzoefu ni muhimu wakatembelea maeneo ya vijijini na kushauri vema wakulima ili kuongeza uzalishaji.

Aidha Padre huyo ameomba kuongezwa vya vitendea kazi ikiwemo matrekta yatakayowezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa. Kuhusu mazingira Padre Laswai amesema mkoa huo unakabiliwa na imani potofu za uchomaji misitu kwa kudhani anaechoma anaweza kuishi muda mrefu hali inayopelekea kuharibu mazingira pamoja na miundombinu ya umeme.

Makamu wa Rais amewataka wananchi wa kijiji hicho kuwalea watoto wao kwa maadili na nidhamu ili kupata taifa lililobora kwa sasa na baadae. Amesema wananchi wa Kijiji hicho wanapaswa kuiga mfano wa maisha ya hapo awali ambayo yalikuwa ni kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuzingatia suala la elimu kwa watoto.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa waumini hao kubadilika mara moja na kuacha tabia za kuharibu misitu kwa kuichoma moto kwa imani zisizofaa. Ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Buhigwe kusimamia kikamilifu sheria ndogo za kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha wote wanaoharibu mazingira wanachukuliwa hatua.

Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kasumo kujitolea kwa hali na mali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini hapo pamoja na kuwaasa viongozi  serikali ya kijiji kuendelea kutoa ardhi kwaajili ya ujenzi huduma za  kijamii kama vile shule na zahanati.

About the author

mzalendoeditor