Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA AITAKA RUWASA KUJITATHMINI KATIKA KUSIMAMIA MRADI WA MAJI ROMBO

Written by mzalendoeditor

Na Mathias Canal, Rombo

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kujitathmini kutokana na kadhia ya kushindwa kusimamia mradi wa maji Wilayani Rombo.

Mbunge wa Jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prf Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo  wakati akiwa katika muendelezo wa ziara jimboni humo ambapo amekagua ujenzi wa mradi wa maji wa Bilioni 2.9

Prof Mkenda amekagua mradi huo ambao mkandarasi alisaini kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka huu 2022 lakini mpaka sasa hakuna kazi iliyokwisha kufanyika zaidi ya kuwekwa mchanga na kokoto zisizozidi hata gari moja.

Prof Mkenda amesema kuwa ameamua kufika na kukagua chanzo cha maji katika mto Wona ambapo mradi huo utakapokamilika utarahisisha upatikanaji maji kwa lita Milioni 4 kwa siku na kupunguza kwa kiasi kikuwa tatizo la maji Rombo linaloikabili Wilaya ya Rombo.

“Tatizo namba moja, mbili, na tatu Rombo ni maji sasa mtu anayechezea mradi wa maji sielewi ana madhumuni gani na anataka wananchi wa Rombo wawe na taswira gani kwa serikali, wanamhujumu Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso ambaye ni mchapakazi na kwa hili nitamualika aje aone changamoto hii” Amekaririwa Prof Mkenda

Amesema kuwa Mradi huo ni sehemu ya miradi ya maji yenye jumla ya Bilioni 10 iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya maji Wilayani Rombo.

“Kwa kuwa sehemu hiyo ni ngumu kufika sio rahisi kwa viongozi kufika na kuona maendeleo ya mradi huo inakuwa rahisi kuficha mapungufu haya kwahiyo RUWASA inabidi ijiangalie upya kwa kuwa ndio msimamizi wa mradi huo” Amesisitiza Prof Mkenda

Mhe Prof Adolf Mkenda ambaye ni mbunge wa Jimbo la Rombo Mkoani Kilimanjaro amesema kuwa kwa sasa katika Wilaya ya Rombo, RUWASA inatia shaka usimamizi wake wa miradi ya maji hvyo amemuomba Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo kutembelea Rombo ili kujionea kadhia hiyo ya ucheleweshwaji wa mradi wa maji.

About the author

mzalendoeditor