Featured Kitaifa

UJUMBE WA WATAALAMU WIZARA YA ELIMUMSINGI YA AFRIKA KUSINI WATEMBELEA SHULE YA MSINGI CHIEF ALBERT KUTHULI MOROGORO

Written by mzalendoeditor

Ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Elimumsingi ya Afrika Kusini umetembelea shule ya Msingi Chief Albert Luthuli iliyopo Mazimbu Mkoani Morogoro.

Shule hii iko katika moja ya eneo waliloishi wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini wakati wa harakati za ukombozi wa nchi hiyo.

Akiwa Shuleni hapo Mkuu wa Msafara huo, Enoch Rabotapi ambaye ni Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu nchini humo (Chief Director Teacher Development) ameahidi ushirikiano kati ya shule hiyo na baadhi ya shule zitakazobainishwa nchini Afrika Kusini kwa kubadilishana uzoefu na walimu.

“Uhusiano wa nchi ya Tanzania na Afrika ya Kusini ni wa muda mrefu, na itakumbukwa mwaka 2018 Rais wetu wa Afrika Kusini akiwa nchini Tanzania aliahidi kutembelea shule hii. Na hivi juzi Mwezi huu wa Julai Waziri wetu wa Elimu ya Msingi nae alitoa ahadi na ndio maana tupo hapa. Tumefurahi kwa kweli, kikubwa tunaahidi kushirikiana kuendeleza shule hii,” amesema Mkurugenzi huyo.

Akizungumza kabla ya kuanza ziara katika Shule hiyo Sylvia Lupembe, Mkuu wa Mawasiliano Serikalini Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Ujumbe huo uko nchini kuungana na watalaamu wa elimu wa hapa nchini na wa Kiswahili kwa ajili kuandaa Mpangokazi wa Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika kuendeleza elimumsingi ikiwemo ufundishaji Kiswahili nchini Afrika Kusini.

Hati hiyo ilisainiwa na Mawaziri wa Elimu wa nchi hizo mbili Jijini Dar es Salaam Julai 7, 2022 ambayo ilikuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chief Albert Luthuli, Theresia Swai ameishukuru nchi ya Afrika Kusini kwa kuendeleza ushirikiano na nchi Tanzania na kuthamini mchango wa nchi yetu katika harakati za ukombozi wa nchi yao.

About the author

mzalendoeditor