Sehemu ya shamba la mikorosho linalomilikiwa na Jeshi la kujenga Taifa kupitia shirika la uzalishaji mali la Suma Jkt lenye ukubwa wa ekari 1,280 wilayani Tunduru.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro(hayupo pichani)wakati akizungumza katika ufunguzi wa shamba la kilimo na mifugo la Jeshi la kujenga Taifa lililopo wilayani humo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Wakili Julius Mtatiro,akizungumza na maafisa,askari wa Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya ufunguzi wa shamba la kilimo na mifugo linalomilikiwa na Jeshi hilo,katikati Mwakilishi wa mkurugenzi wa Suma Jkt Meja Peter Kulyakwave na kushoto Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro wa pili kushoto,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Chiza Marando wa kwanza kushoto na Mtaalam wa kilimo na kifugo wa Suma JKT Meja Peter Kulyakwave wa pili kulia wakikagua sehemu ya shamba la mikorosho la Jeshi hilo,wa kwanza kulia kaimu kataibu tawala wa wilaya Asia Lugomi.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kushoto akiondoa kitambaa kama ishara ya ufunguzi rasmi wa shamba la kilimo na mifugo la Jeshi la Kujenga Taifa JKT,kulia mtaalam wa kilimo na mifugo wa SumaJkt Meja Peter Kulyakwave na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni Tanzu ya SumaJKT Ports &Services Meja Joseph Marwa.

……………………….

Na Muhidin Amri,

Tunduru

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Wakili Julius Mtatiro,amezindua mradi mkubwa wa shamba la kilimo na ufugaji la Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) lenye ukubwa wa ekari 1,280 wilayani humo.

Shamba hilo, linasimamiwa na Kampuni Tanzu ya Suma JKT ijulikanayo kama Suma JKT Ports &Services Co. Ltd linatumika kwa kilimo cha zao la korosho,ufugaji wa kuku wa mayai na nyama,mbuzi na ng’ombe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba hilo,Mtatiro amempongeza Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele na Mkurugenzi wa Suma JKT Kanali Petro Ngata kwa kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Jeshi hilo ikiwamo kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya ya Tunduru, ameitaka Suma JKT kuendelea kupanua wigo wa shughuli zake hasa katika sekta ya kilimo cha korosho kwa kuwa wilaya hiyo ina maeneo makubwa yanayofaa kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali.

Mtatiro alisema kuwa,katika wilaya ya Tunduru kuna hazina kubwa ya ardhi inayofaa kwa kilimo,ambapo hadi sasa ardhi iliyotumika kwa shughuli za kilimo na ufugaji ni asilimia 20 ambapo asilimia 80 zilizobaki, asilimia 60 kwa ajili ya wananchi na ishirini zimetengwa kwa ajili ya taasisi mbalimbali za serikali.

Alisema, shamba hilo linalomilikiwa na SUMA JKT lina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 600 ya korosho,hata hivyo uzalishaji huo utafikiwa iwapo itapandwa miche ya kisasa na kusimamiwa vizuri, badala ya kutegemea miche ya zamani ambayo uzalishaji wake ni mdogo.

Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Marando, kukaa na wataalam wake na kupitia maeneo yote yaliyotengwa kwa kwa ajili ya mpango maalum wa kilimo(Block Farming)na kuwashiriki Suma Jkt ili maeneo hayo yaweze kufanyiwa kazi ili kutimiza malengo ya Serikali.

Mtatiro,amewaasa wananchi hasa wakulima na wafugaji,kwenda kujifunza namna ufugaji bora na kilimo cha kisasa kwenye shamba hilo ili waweze kupata mafanikio kupitia sekta hizo,badala ya kuendelea kufuga na kulima kizamani.

Aidha,amewataka watu wanaotaka kuingiza mifugo katika wilaya hiyo kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu kwa kupeleka mifugo yao kwenye maeneo yaliyotengwa(vitalu) badala ya kuzurura ovyo ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kati ya wakulima na wafugaji.

“kiasili wananchi wa Tunduru sio wafugaji,lakini kuna watu wanaotoka nje ya wilaya hiyo na kuingiza idadi kubwa ya mifugo, hata hivyo kutokana na uwekezaji unaofanywa na Suma JKT ni muhimu kwenda kujifunza namna bora ya ufugaji wa kisasa na kuepuka kuzurura na makundi makubwa ya mifugo porini”alisema Mtatiro.

Pia,ametoa siku kumi na nne kwa shirika la umeme Tanesco na Wakala wa usambazaji maji vijijini(Ruwasa) wilayani humo, kupeleka mpango wao wa kazi ofisini kwake kuhusu maandali ya kupeleka umeme na maji katika shamba hilo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la uzalishaji mali la Suma JKT Meja Dkt Peter Kulyakwave alisema,shirika la Suma JKT linatekeleza mkakati wake wa kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.

Alisema, Suma Jkt imejipanga kujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwamo kilimo na ufugaji katika shamba hilo kwa kupanda mikorosho mipya,kufuga ng’ombe na kuwanenesha kwa kuwapa chakula na virutubisho vinavyohitajika kabla ya kupelekwa sokoni kuuzwa.

Meja Kulyakwave alisema, shamba hilo la kilimo na mifugo Tunduru litakuwa sehemu ya mafunzo kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji ili waweze kuongeza thamani ya mazao wanayolima na mifugo na hatimaye kupata bei nzuri wanapofikisha sokoni.

Alieleza kuwa,matarajio ya shirika la uzalishaji mali la Jeshi la kujenga Taifa (SUMA JKT) kwamba shughuli zote za kilimo na ufugaji zinazofanyika katika shamba hilo zitaongeza ufanisi katika utendaji wa kampuni kwa kupunguza baadhi ya changamoto na kuongeza wigo wa mapato.

Amemuagiza Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya SUMA JKT Ports & Services, kutoishia kwenye ufugaji na kilimo tu bali kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao yatakayozalishwa katika shamba hilo na wananchi.

Kwa mujibu wa Meja Marwa,lengo ilikuwa ni kulinda eneo hilo na pia kuendesha shughuli za kilimo cha zao maarufu  la korosho ambapo JKT kupitia Shirika la uzalishaji mali la SumaJKT lilianza kukalia eneo hilo mwaka 2019 ambapo kampuni tanzu ya SUMAJKT Ports &Services ilikabidhiwa jukumu  la kusimamia na kuendesha shamba hilo.

Alisema,baada ya kukabidhiwa Kampuni iliweka mpango wa kuliendeleza shamba  ikiwamo kujenga jengo la kukaa vijana,kutunza mikorosho iliyopo,kusafisha shamba kwa awamu na kupanda mikorosho mipya.

Meja Marwa alieleza kuwa,mwaka 2022 JWTZ iliamua kuchukua eneo hilo tena kwa shughuli za kiusalama na kuacha zaidi ya ekari 700 ambapo tayari Suma Jkt lilikuwa limeanza kuziendeleza kwa shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji.

Alisema,mpaka sasa Suma JKT Ports &Services imefanikiwa kusafisha shamba lote,kupana miche mipya 300 ya mikorosho ya muda mfupi,kuhakiki mipaka ya shamba na baada  uhakiki uliyofanywa kwa kushirikiana na ofisi ya Ardhi Wilaya na kamati ya ulinzi na usalama imebaini shamba hilo lina ukubwa wa ekari 2,180.

Aliongeza kuwa,kampuni imeanza kuendesha shughuli  mbalimbali ikiwamo ufugaji  wa kuku wa kienyeji 200 na vifaranga 234,mbuzi 60,ng’ombe wa kunenepesha 20,ulinzi wa mipaka ya eneo na kujenga nyumba  kupokea umeme(Power Hause).

Previous articleOFISI YA MKUU WA MKOA DODOMA YAPOKEA HATI YA USHINDI WA USAFI WA OFISI ZA WAKUU WA MIKOA NCHINI
Next article RAIS MUSEVENI WA UGANDA NA RAIS NDAYISHIMIYE WA BURUNDI WAONDOKA NCHINI,WAZIRI MKENDA AWAAGA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here