Featured Kitaifa

SIMBACHAWENE:’KAMPENI GGM KILI CHALLENGE IMESAIDIA MAPAMBANO YA KUDHIBITI UKIMWI

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene (wa pili kushoto) akimkabidhi mmoja wa washiriki wanaopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya VVU kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge 2022. Kushoto ni Mkurugenzi wa TACAIDS Dk. Leonard Maboko.

……………………………………

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema jitihada za Kampeni ya GGM Kili Chalenge pamoja na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali, zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na VVU/Ukimwi kwa asilimia 50 kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.

Pia amesema maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020 wakati maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.

Simbachawene ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akiwaaga wapanda mlima Kilimanjaro 52 ambao kati yao 28 wanauzunguka mlima kwa baiskeli na 24 kwa kutembea kwa miguu.

Zoezi hilo lililoanza Julai 15, 2022, linaratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa ukimwi. Wapanda mlima hao, watashuka Julai 21 mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine Simbachawene alisema serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa afua zinazotekelezwa za mwitikio wa VVU na UKIMWI zinaleta tija kwa makundi mbalimbali katika jamii.

Alisema ili kufikia malengo haya pamoja na mengine katika kuishinda vita hii dhidi ya VVU na UKIMWI, kunahitaji nguvu ya pamoja kati ya serikali na wadau wengine, hususan sekta binafsi ili kupata rasilimali fedha ya kutosha.

 “Kili challenge inalenga kupunguza athari za kupungua kwa misaada ya wahisani na kuiwezesha Nchi kuimarisha uwezo wa ndani kwa ajili ya kudhibiti UKIMWI”

Aidha, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimami miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli zaidi ya 700 kutoka mabara 6 na zaidi ya nchi 20.

Alisema kupitia kampeni ya hiyo, taasisi mbalimbali zimenufaika kwa kupata fedha za kutekeleza shughuli za mwitikio wa VVU na Ukimwi nchini.

“Kwa mfano, mwaka 2020 Mfuko wa Kilimanjaro Challenge ulitoa fedha taslim milioni 800 kwa taasisi 20 zisizo za kiserikali.

“Tunawakaribisha sana wadau na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki katika kampeni hii,” alisema Shayo.

Aidha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko, alisema kwa muda wa miaka 20 tangu kampeni hiyo ianzishwe zaidi ya Sh bilioni 11 zimekusanywa na kusaidia katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Alisema licha ya maendeleo mazuri yatokanayo na jitihada hizo, bado kuna maeneo ambayo yanahitajika nguvu zaidi ili kudhibiti VVU na UKIMWI na hatimaye kutokomeza VVU/UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kama inavyoelekezwa katika malengo ya kidunia.

“Mojawapo ya malengo hayo ni kuzuia maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana kwani zaidi ya theluthi moja ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24, hususan vijana wa kike,” alisema.

About the author

mzalendoeditor