Featured Kitaifa

TANZANIA YA TANO AFRIKA KUZALISHA MIONZI DAWA

Written by mzalendoeditor

Na.Catherine Sungura,Siha

Tanzania ni kati ya nchi tano Afrika na ni nchi pekee Afrika Mashariki inayozalisha mionzi dawa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri na Mbunge wa jimbo la Siha Dkt. Gwodin Mollel wakati wa ufunguzi wa Maabara ya Afya ya Jamii iliyoko katika hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto iliyofunguliwa na Makamu wa Rais Mhe.Philip Mpango

Alisema hatua hiyo imetokana na uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Dkt. Mollel alisema uwekezaji huo umeweza pia kuifanya Tanzania kuwa na uwezo wa kupasua vivimbe vya ubongo bila kupasua kichwa na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali ambazo ilikua inazipata kwa kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi ikiwemo India.

Alitolea mfano kwa upasuaji wa vivimbe vya ubongo kwa nje ya nchi kwa mgonjwa mmoja ilikua ikigharimu Milioni 90 lakini kwa hapa nchini upasuaji kama huo unafanyika kwa Milioni 8.

Kwa upande wa kupandikiza Uloto Dkt. Mollel alisema kwa mgonjwa mmoja nje ya nchi Serikali ilikua ikilipa Milioni 250 lakini kwa sasa hapa nchini upandikizaji huo unafanywa kwa Milioni 70 na hivyo kuokoa kiasi cha shilingi Milioni 180.

About the author

mzalendoeditor