Mgeni-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania Jimbo La Iringa Blaston Gaville wakati wa sherehe za siku ya Chuo Kikuu cha Iringa iliyofanyika jana tarehe 14 Julai 2022 Mjini Iringa.
Na Mathias Canal, WEST-Iringa
Serikali imesema kuwa haitafanya
uzembe kwenye usimamizi wa Ubora wa elimu nchini hivyo imeitaka Tume ya Vyuo
Vikuu (TCU) kuhakikisha kuwa inaendeleza udhibiti wa ubora wa elimu nchini
katika ngazi ya vyuo vikuu nchini.
TCU imekumbuswa lengo la kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja
kuhakikisha inasimamia kwa weledi mkubwa elimu ya vyuo vikuu nchini kwa
kufanya utambuzi na uidhinishaji wa elimu ya vyuo vikuu kabla ya chuo kikuu chochote kuanza.
Akizungumza jana
tarehe 14 Julai 2022 wakati wa sherehe za siku ya Chuo Kikuu cha Iringa Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa hakutakuwa na shinikizo lolote la utoajia wa Digrii
zisizokidhi vigezo kwenye kazi za kitaaluma hivyo serikali itahakikisha kuwa
ubora wa elimu unasimamiwa ipasavyo.
Waziri Mkenda amesema kuwa ili kuwe
na wataalamu wazuri katika sekta ya afya ni vyema kama kuna uwezekano vigezo
viongezwe hususani katika usimamizi wa maswala ya tiba ili kuakisi ubora wa
elimu nchini.
“Tukicheza na ubora wa elimu
tutaua nchi yetu, na hapa nchini vipo baadhi ya vyuo vya binafsi ambavyo ili
viwe na wanafunzi wengi vinatoa GPA kubwa pasina kujali ubora na uwezo wa
wahitimu wao” Amekaririwa Prof Mkenda na kuongeza kuwa
“Tanzania sio kapu la kutuletea
Digrii feki hivyo ubora wa elimu utasimamiwa bila woga na presha ya watu wenye
fedha au wana siasa, lakini na nyie TCU mtoe majibu kwa wakati mkichelewa
hatutaelewana”
Prof Mkenda amesema kuwa Vigezo vya
udahili na utoaji elimu vinafahamika, ubora unafahamika, hivyo tathmini
ikifanyika vikaangaliwa vigezo kila mtu atapata kwa mujibu wa vigezo hivyo na
si vinginevyo.
“Nchi yetu haiwezi kuendelea
kwa kupeana nafasi kwa undungu, na kwa upendeleo ila tunaweza tukaendelea
tukipeana nafasi kwa uwezo, vipaji na juhudi sio kwa sababu baba yako ana hela
nyingi ndio upewe hiyo Hapana” Amesisitiza Prof Mkenda
Waziri Mkenda amesema unaweza kuwa
na akili nyingi lakini mvivu na mlevi, una uwezo mkubwa lakini mzembe hivyo
lazima TCU isimamie ubora na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili elimu ya
Tanzania isiwe ni bora elimu bali elimu yenye ubora.