Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU ATINGA MKIWA

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,ameendelea na ziara yake ya kata kwa kata ambapo Julai 14,2022,ametembelea kijiji cha Choda kilichopo Kata ya Mkiwa.

Lengo la ziara hiyo ni kuwapatia wananchi mrejesho wa bunge la bajeti, kuhamasisha sensa ya watu na makazi ,kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akizungumza na wananchi hao,Mtaturu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo kazini na ina dhamira ya kuendeleza yale yote yaliyoanzishwa na awamu ya tano na kuanzisha mengine mapya.

Amesema katika bajeti ya mwaka huu kata ya Mkiwa itafaidika na ujenzi wa Barabara ya Mkiwa-Choda ambayo imetengewa Sh Milioni 150 na Barabara ya Mkiwa-Damaida imetengewa Sh Milion 160 kwa ajili kupandisha tuta na kujenga karavati ambapo kwa sasa zipo kwenye hatua za manunuzi ili apatikane mkandarasi na ujenzi uanze.

“Upande wa maji tumeshaleta wataalam kupima maeneo ya kuchimba kisima kirefu ili baadae tusambaze maji hadi kwenye taasisi ya shule ya msingi Choda ambapo serikali ilileta Sh Milioni 18 kwa ajili ya kujenga vyoo vya kisasa matundu 10 ila changamoto iliyokuwepo ni maji ya kutumia kwenye vyoo hivyo,”amesema.

Amewaomba wananchi wa Choda na Mkiwa kuishi kwa upendo na washirikiane ili kuharakisha maendeleo yao.

“Niwaombe pia ndugu zangu tushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi litakayofanyika tarehe 23 August 2022 kwa maendeleo ya Taifa letu,kila mmoja ashiriki zoezi hili na atoe taarifa sahihi ili kusaidia serikali kupata takwimu zetu na hivyo kuharakisha maendeleo yetu,”ameongeza.

Ziara hii maarufu kama
*”HUDUMA JIMBONI”* ikiwa imefika siku ya tatu tayari imefika katika kata za Mang’onyi,Unyahati na Mkiwa na vijiji vya Mbogho,Mang’onyi,Kinyamwadyo,Matare,Choda na Mkiwa lengo likiwa ni kufika katika kata na vijiji vyote vilivyopo katika jimbo hilo,hakika hakuna jiwe ambalo halitageuzwa.

#Huduma jimboni
Singida Mashariki
#SENSA 2022,Jiandae jitokeze kuhesabiwa ewe
Mwana Singida Mashariki.

About the author

mzalendoeditor