Featured Kitaifa

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI ZINAZOTOA ELIMU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Na WyEST_Iringa

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na kuziwezesha Taasisi za umma na binafsi zinazotoa elimu nchini ili kuhakikisha zinatoa elimu bora inayolenga taaluma na ujuzi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda (Mb) leo Julai 14, 2022 mjini Iringa katika maadhimisho ya siku ya Chuo Kikuu cha Iringa ambapo imeitaka Tume ya Vyuo Vikuu nchini kuwa imara katika kusimamia ubora na kuwa haitaingiliwa katika kazi hiyo.

Mkenda amesema Serikali pia imekuwa ikiwezesha wanachuo wa Vyuo vyote vikiwemo vya umma na binafsi kupata mikopo bila kubagua.

Ameongeza kuwa mbali na mikopo hiyo kwa mara ya kwanza Serikali imetenga fedha kiasi cha Shilingi bilioni tatu katika bajeti ya Mwaka 2022/23 kwa ajili ya kutoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi waliofanya vizuri sana katika masomo ya sayansi kidato cha sita watakaodahiliwa na vyuo vikuu nchini kusomea Shahada za Uhandisi, Sayansi na Elimu tiba ambapo takriban wanafunzi 500 watapata udhamini huo.

Aidha Serikali pia kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) inakwenda kutoa udhamini wa masomo kwa Wahadhiri kutoka taasisi za elimu ya juu za Serikali na binafsi katika vyuo mbalimbali vya nje ya nchi ili kuongeza idadi ya Wahadhiri wenye taaluma na uzoefu kutoka nje ya Tanzania.

“Serikali katika kutoa fursa za upatikanaji wa elimu bora nchini haiangalii vyuo vya Serikali pekee bali inatoa fursa hizo sawa kwa kuwa taasisi binafsi za elimu pia zinatoa elimu kwa watoto wa Kitanzania hivyo suala la kuwezesha ni jambo muhimu ambalo Serikali haiwezi kuacha kufanya,” amefafanua Prof. Mkenda.

Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu juu, Waziri Mkenda amewataka wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na masomo kwa mwaka 2022/23 kusoma kwa umakini Mwongozo wa Uombaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu na kuomba ushauri kabla ya kujaza fomu za uombaji mikopo hiyo ambapo amesema mara nyingi wahitaji hukosa mikopo hiyo kwa sababu tu fomu zao hazijajazwa kwa umakini.

Aidha ameongeza kuwa Serikali imeunda timu ya watu watatu wa kufanya mapitio ya mfumo mzima wa utoaji mikopo ili kuhakikisha mikopo hiyo haitolewi kwa upendeleo na kwamba inatolewa kwa wahitaji wa ukweli.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa, Prof. Ndelilio Urio amemweleza Waziri Mkenda kuwa mfumo wa ufundishaji wa kutumia nadharia na vitendo ili kuwapatia ujuzi wanafunzi uliigwa kutoka nchini Finland na unawezesha wahitimu wanaomaliza masomo yao kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika jamii.

Prof. Urio amesema wanahakikisha mfumo huo unakwenda sambamba na vigezo vilivyowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kueleza kuwa chuo kinashirikiana kwa karibu na TCU katika kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo la KKKT Iringa Prof. Blaston Gavile ameishukuru Serikali kwa kukisaidia chuo hicho pale kinapoomba msaada ambapo amesema iliwezesha chuo hicho kuungwa katika Mkongo wa Taifa pamoja na kupata mkopo wa fedha kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Ameongeza kuwa Serikali pia imewezesha Chuo hicho kupata vifaa vya TEHAMA kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na kuwa Chuo kikuu cha Kwanza nchini kuunganishwa na Mkongo wa Taifa.

About the author

mzalendoeditor