Kitaifa

ZAIDI YA BIL. 37 ZATUMIKA KIWANJA CHA NDEGE CHA SONGEA 

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Ephatar Mlavi kuhusu maendeleo ya upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha SOngea, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo yake Mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Ephatar Mlavi (wa pili kushoto) na Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songea, Jafari Mbana (kulia), wakati alipokagua kiwanja hicho Mkoani Ruvuma.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa jengo la muda la kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Songea, mkoani Ruvuma. Jengo hilo ni sehemu ya mradi wa upanuzi wa kiwanja hicho ambao umegharimu kiasi cha shilingi takribani bilioni 37 na unatarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu.

Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami katika Kiwanja cha Ndege cha Songea Mkoani Ruvuma. Barabara hiyo imeongezwa urefu kutoka mita 16625 hadi 1860 na mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu.

PICHA NA WUU

…………………………………………..

Kukamilika kwa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea uliogharimu takribani shilingi bilioni 37 kutawezesha ndege sita za kubeba abiria takribani 70 kuhudumiwa kwa wakati mmoja kwa saa 24 siku saba za wiki. 

Akizungumza mkoani Ruvuma mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi wa kiwanja hicho, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema Serikali iliangalia fursa zilizopo mkoani humo ikiwemo uchimbaji wa Makaa ya Mawe, Utalii, Kilimo na kuamua kuboresha kiwanja hicho ili kurahisisha biashara na shughuli za usafirishaji na uchukuzi. 

“Mkoa huu una fursa nyingi hivyo kama Serikali tukaona tuboreshe kiwanja hiki ili wafanya biashara, wawekezaji na wananchi waweze kuwa na urahisi wa usafiri kwani biashara huwa hazina mipaka zinaweza kufanyika saa 24″, amesema Naibu Waziri Mwakibete. 

Naibu Waziri Mwakibete, amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwa na maono ya kuboresha kiwanja hicho kufikia kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 300. 

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewapongea TANROADS na TAA kwa kuhakikisha mkandarasi anazingatia thamani ya fedha na viwango kwenye ujenzi wa kiwanja kwa kumsimamia kwa karibu. 

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Eng. Ephatar Mlavi, amesema kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 90 na kazi zinazoendelea ni pamoja na kukamilisha jengo la muda la kuongozea ndege na usimikaji wa taa kwenye barabara ya kuruka na kutua ndege. 

Mhandisi Mlavi ameongeza kuwa kiwanja hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti ambapo mkandarasi anatarajia kukikabidhi kazi zote mwezi Septemba mwaka huu. 

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songea, Jafari Mbana, amesema kukamilika kwa upanuzi huo kumeongeza safari za ndege hususani kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwani imeongeza safari zake kutoka safari mbili mpaka tatu kwa wiki. 

Upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Songea  umehusisha barabara ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 1625 hadi mita 1860 na upana mita 30, ujenzi wa uzio, jengo la muda la kuongozea ndege, maegesho ya ndege, taa, gari la zimamoto na mifumo mbalimbali. 

About the author

mzalendoeditor