Featured Kitaifa

AJALI YAUA WATANO MKOANI SIMIYU

Written by mzalendoeditor

Watu watano wamefariki dunia na wengine 11 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Magereza nje kidogo ya mji wa Bariadi Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu usiku wa kuamkia leo Jumatano Julai 13, 2022.

Ajali hiyo imetokea siku moja baada ya ajali nyingine kusababisha vifo vya watu wanane wakiwamo watano wa familia moja iliyotokea katika barabara kuu ya kutoka Lusahunga kwenda Nyakahura wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso.

Akizungumza na waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya mji wa Bariadi, Somanda Emmanuel Constantine amethibitisha kupokea miili ya watu wanne na majeruhi wanne.

Ajali hiyo ilihusisha magari madogo mawili ya abiria aina ya Toyota pro box yenye na Toyota wish ambayo yanayofanya safari zake kati ya mji wa Bariadi na Lamadi wilayani Busega ambayo yaligongana uso kwa uso.

“Majeruhi tuliowapokea wamepata majeraha kwenye migongo na hali zao zinaendelea vizuri na hadi sasa wanaendelea kupatiwa matibabu hapa hapa hospitalini” amesema Dk Constantine.

Chanzo:Mwananchi

About the author

mzalendoeditor