Featured Kitaifa

TAEC YATAJA SABABU ZA KUDHIBITI MIONZI KWENYE MNYORORO WA BIDHAA

Written by mzalendoeditor

Mtafiti wa Tume ya Nguvu za Atomic Bw. Vitus Abel akitoa maelezo Kwa wananchi mbalimbali waliotembelea katika banda la taasisi hiyo kwenye maonesho ya 46 ya biashara ya Kimataifa viwanja wa Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Mtafiti wa Tume ya Nguvu za Atomic Bw. Alex  Muhulo  akitoa maelezo Kwa wananchi mbalimbali waliotembelea katika banda la taasisi hiyo kwenye maonesho ya 46 ya biashara ya Kimataifa viwanja wa Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Peter Ngamilo amesema, kuna sababu nyingi na faida za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kwa kuwa matumizi ya bidhaa hizo zenye viasili vya mionzi ni hatari kwa afya.

Ameyasema hayo akiwa katika Maonesho ya 46 ya Kimaiafa ya Dar es Salaam maarufu sabasaba yanayoendelea, viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa, Jijini Dar es Salaam ambapo TAEC inashiriki kutoa elimu kwa Umma juu ya namna inavyotekeleza majukumu yake kisheria hapa nchini.

Bw. Ngamilo amebainisha kuwa TAEC wamejizatiti katika udhibiti wa matumizi salama ya mionzi, uhamasishaji na uendelezaji wa teknolojia ya nyuklia katika baadhi ya sekta za afya, mifugo, maji, kilimo, madini, viwanda.

Akibainisha sababu za msingi za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa Bw. Ngamilo amesema wanatoa elimu hiyo,kwa sababu wananchi walio wengi wamekuwa na shauku ya kujua kwa nini TAEC wanadhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa.

“Amesema, mionzi ina faida nyingi na inachangia mambo mengi muhimu katika ustawi wa jamii lakini ikitumika ndivyo sivyo madhara yake kiafya ni makubwa hivyo udhibiti wa hali ya juu ili kuhakikisha matumizi salama ni lazima uzingatiwe.

Katika sekta ya afya mionzi hutumika katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, kwenye Sekta ya Kilimo mionzi huwa inatumika katika kutafuta upatikanaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali na kwenye Sekta ya Mifugo hutumika kutokomeza wadudu waharibifu kama ambavyo ilifanyika katika kuteketeza mbung’o kule Zanzibar.

Pia amesema, mionzi hutumika kwenye sekta za ujenzi kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa reli, ujenzi wa mindombinu ya bomba la mafuta na katika suala zima la utafiti kwenye vyuo vikuu na maeneo mengine yanayofanya utafiti
Amesema, kuna sababu nyingi za kudhibiti mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama safirishaji holela wa vyanzo vya mionzi unaweza kupelekea uchafuzi wa mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa na endapo wananchi wakizitumia bidhaa hizo zenye viasili vya mionzi matokeo ni kupata magonjwa ya saratani na kuharibu mfumo wa Vinasaba (DNA).

“Hivyo kama taasisi yenye jukumu la kudhibiti matumizi ya mionzi lazima tuhakikishe wananchi, mazingira, wagonjwa na wafanyakazi wanaotumia vyanzo vya mionzi kutoa huduma mbalimbali wanakuwa salama dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kupitia mionzi.

“Sababu nyingine ya uwepo wa mionzi ya asili kwenye udongo na mazingira yetu kwa sababu nchi yetu katika maeneo mengi ina madini ya urani, hivyo ni jukumu letu kama taasisi ya kudhibiti na kuweza kuchukua sampuli mbalimbali za kimazingira na mimea ili kupima na kuangalia viasili vya mionzi vilivyomo, hii yote ni katika kuhakikisha tunawalinda watanzania dhidi ya madhara mabaya ya mionz,”amesema.

Ametaja sababu nyingine kuwa, ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi dhidi ya uchafuzi wa mnyororo wa bidhaa.

Bw.Ngamilo amesema kutokana na majukumu hayo, kwasasa TAEC ina ofisi 30 nchi nzima huku lengo ni kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya madhara yatokanayo na mionzi lakini pia kurahisisha biashara kwa wafanyabiashara wote nchini.

Sababu nyingine, Bw.Ngamilo amesema kuwa, ni kuhakikisha wanalinda soko la bidhaa nje ya nchi kwani kwa sasa kuna vita kubwa ya kiuchumi hivyo ni jukumu la serikali kulinda masoko ya bidhaa za Tanzanaia nje ya nchi ili isije ikatokea mtu mwenye nia ovu kuweka viasili vya mionzi kwenye bidhaa na hatimaye tukapoteza soko la bidhaa zetu nje ya nchi.

Sababu nyingine ni kutimiza matakwa ya Sheria namba 7 ya Nguvu za Atomiki ambayo inawataka kudhibiti, Sheria za kimataifa kama Sheria ya Shirika la Afya Duniani (WHO),Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) ambapo Tanzania ni wanachama.
“Hizi ni baadhi ya sababu za msingi zinazotufanya sisi kama Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania tuweze kudhibiti mionzi katika mnyororo wa bidhaa,”amesema Ngamilo.

About the author

mzalendoeditor