Featured Kitaifa

KIWANJA CHA NDEGE CHA MTWARA KUKAMILIKA MWEZI SEPTEMBA

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John kuhusu maendeleo ya upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Mtwara, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja hicho.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa uongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Mtwara na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), alipokagua maendeleo ya Kiwanja hicho Mkoani Mtwara.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) Mkoa wa Mtwara, Christopher Lyimo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo kiwanjani hapo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kiwanja cha Mtwara

PICHA NA WUU.

……………………………………..

Imeelezwa kuwa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Septemba mwaka huu ili kuruhusu ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 250 kuweza kuruka na kutua kiwanjani hapo. 

Akizungumza mkoani humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi huo Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amefafanua kuwa kiwanja hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege hizo kwa saa 24 siku saba za wiki. 

“Nawapongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), na Mamlaka ya Viwnja vya Ndege Nchini (TAA), kwa kuendelea kumsimamia kwa karibu mkandarasi anayejenga kiwanja hiki ni imani yangu kitakamilika kwa viwango bora na kutaruhusu ndege kubwa kutua na kitafanya kazi saa 24″, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete. 

Naibu Waziri Mwakibete amezitaka Taasisi hizo kupunguza urasimu pale mkandarasi anapowasilisha madai yake kwani matokeo ya kuchelewesha malipo ni pamoja na Serikali kulipa madeni na kuchelewesha kukamilika kwa mradi. 

“Siku zote tusijisahau kama hati ya madai imekuja mapema nasi kama Serikali tuwe tunazipitisha maeneo zinapotakiwa kupita kwa wakati na malipo yafanyike ili kuepusha mkandarasi kudai tunapochelewesha kumlipa’ amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mtwara, Eng. Dotto John, amesema upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia  92 na kwa sasa kazi zinazoendelea ni pamoja na kutayarisha miundombinu ya taa na zoezi hilo litakamilika ndani ya mwezi mmoja. 

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja hicho, Samuel Mrumi, amesema awamu ya kwanza ya upanuzi wa kiwanja hicho umehusisha kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 2,258  hadi 2,800 na upana kutoka mita 30 hadi 45, eneo la maegesho ya ndege, uwekaji wa taa, gari la zima moto na ujenzi wa uzio. 

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku mbili ambapo anakagua miundombinu na miradi ambayo inatekelezwa na Wizara kupitia Taasisi za Sekta ya Uchukuzi. 

About the author

mzalendoeditor