Featured Kitaifa

SIMBA GAS YAJIWEKA TAYARI KWA UCHIMBAJI WA GESI YA UKAA BAADA YA KUPOKEA RIPOTI YA UTAFITI KUTOKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Written by mzalendoeditor
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye (wa pili kushoto) akimkabidhi Ripoti ya Utafiti wa Gesi Ukaa, Mkurugenzi Mtendaji wa Simbagas, David Ndelwa (wa pili kulia) kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza uchimbaji wa gesi hiyo mkoani Mbeya, hafla ya makabidhiano ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa kitivo cha Jiolojia na Madini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Elisante Mshiu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera.
**
 
 
Kampuni ya Kitanzania ya Simba Gas, inajiandaa na uchimbaji wa gesi ya ukaa (Carbon dioxide) huku ikilenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya bidhaa hiyo katika soko la ndani na nje.
 
Uchimbaji utaanza baada ya kupata vibali vyote vya udhibiti kutoka katika taasisi zote zinazohusika.
 
Haya yanajiri wakati kampuni hiyo ikipata uhakika wa upatikanaji wa gesi ya ukaa katika eneo la Kata ya Suma lililopo Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya zoezi la utafiti wa miezi miwili lililofanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
 
Simba Gas – ambayo ilisajiliwa mwaka 2021 kama sehemu ya kundi la makampuni ya Simba ikijikita katika kuchimba na kuuza gesi ya ukaa imepokea matokeo ya utafiti kutoka kitivo cha jiologia na Madini cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Nishati na Madini ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mh. Juma Zuberi Homera.
 
Gesi ya Ukaa hutumika katika utengenezaji wa vinywaji vyenye gesi, Pia hutumiwa kama kipoozo katika vizima moto kwa kuingizwa katika vifaa vya uokoaji, uchomelea vyuma katika miradi mikubwa, utengenezaji wa barafu kavu (dry ice) zinazotumika kupozea vinjwaji , ulipuaji wa makaa ya mawe, utengenezaji wa vifaa vya mpira na plastiki, ukuzaji wa mimea katika vitalu nyumba na pia kupunguza nguvu za wanyama kabla ya kuchinjwa.
 
Akiongea wakati wa hafla ya kupokea ripoti ya utafiti, Mkurugenzi wa kampuni Simba Gas ndugu David Ndelwa, alisema soko la gesi ya ukaa linakua kwa kasi kubwa ndani na nje ya nchi. “Kwa sasa, mahitaji ya gesi ukaa katika soko la ndani yanafikia tani 1,060 kwa wiki na tunao upungufu wa tani 360 kwa wiki,” alisema.
 
Vile vile, mahitaji ya soko la mauzo ya nje la gesi ya ukaa kwa sasa ni takribani tani 2,000 ambapo upungufu ni tani 1,460.
 
“Inakadiriwa kuwa hadi sasa, soko la kimataifa la gesi ukaa linafikia thamani ya dola bilioni 10.36. Kampuni yetu imejiandaa vya kutosha na itawekeza kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha kuwa tunatumia rasilimali tulizo nazo ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi,” alisema David Ndelwa
 
David Ndelwa alisema Simba Gas, imefanya utafiti na kuona soko kubwa la gesi ukaa katika nchi za Zambia, Zimbabwe, Congo, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Botswana, Angola, Sudan Kusini, Rwanda na Namibia pamoja na nchi nyinginezo.
 
“tunatambua kwa kusafirisha gesi yetu nje ya nchi, tutaleta fedha za kigeni nchini. Pia tutazalisha nafasi za ajira za moja kwa moja 150 na zingine 300 za muda maalum” alisema.
 
Hata hivyo alibainisha kuwa tafiti zaidi zitalazimika kufanyika ili kukidhi matakwa ya kimataifa ya uvunaji wa bidhaa hiyo na ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri yatakayovutia ufadhili zaidi wa shughuli hizo.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mh. Juma Zuberi Homera, alisema Serikali, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inajitahidi kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya nishati na viwanda miongoni mwa mambo mengine.
 
Aliipongeza Simba Gas kwa kuwekeza Mbeya, na kubainisha kuwa kwa kufanya hivyo, kampuni hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya serikali ya kukuza sekta ya uwekezaji na kuisaidia nchi kukuza uchumi wake.
 
“Mradi huu utakapoanza rasmi, utazalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali za mitaa na kusaidia jamii kupitia mipango ya uwajibikaji kwa jamii,” alisema, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono uwekezaji huo.
 
Naye Mkuu wa kitivo cha Jiolojia na Madini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Elisante Mshiu alisema anawashukuru kampuni ya Simba Gas kwa kuwaamini wataalamu wa ndani ambao wamejikita kuleta ukombozi na mageuzi makubwa ya kufanya tafiti za kimkakati na kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali zake.
 
Simba gesi wamedhubutu kufanya tafiti katika uchimbaji wa gesi ukaa, tunaamini watafungua fursa nyingi pia kwa vijana wetu ambao tunawazalisha wakiwa wamebobea katika kuendesha mitambo ya gesi na itafungua milango ya ajira kwa vijana wetu.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye (wa pili kushoto) akimkabidhi Ripoti ya Utafiti wa Gesi Ukaa, Mkurugenzi Mtendaji wa Simbagas, David Ndelwa (wa pili kulia) kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza uchimbaji wa gesi hiyo mkoani Mbeya, hafla ya makabidhiano ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera na kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Simba, Farid Nahdi(kushoto) ni (Kushoto) ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Angelina Ngalula .
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Simbagas, David Ndelwa, akizungumza wakati wa hafla
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo.

Baadhi ya viongozi wa Serikali kutoka mkoani Mbeya wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo.</div

About the author

mzalendoeditor