Featured Kitaifa

DC ARUMERU ATAKA WANANCHI KUHESHIMU MIPAKA KATIKA VYANZO VYA MAJI.

Written by mzalendoeditor
MWAKILISHI wa Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango, Charles Mungure akishirikiana na viongozi wa kata na mwakilishi wa mkurugenzi wa bodi ya maji ya bonde la mto Pangani Segule Segule, Felista Joseph kuzindua upandaji wa miti katika chanzo cha maji cha Saibara wilayani humo.
MWAKILISHI wa  Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango, Charles Mungure ambaye ni afisa mazingira wa halmashauri ya Meru akiongea katika zoezi la upandaji miti zaidi ya 1500 katika chanzo cha maji cha Saibara.
MWAKILISHI  wa Mkurugenzi wa bodi ya maji ya bonde la mto Pangani Segule Segule, Felista Joseph ambaye ni afisa mazingira wa bonde hilo akitoa taarifa ya chanzo cha maji cha Saibara.
Diwani wa kata ya Akeri Julius Mungure akiongea na wananchi katika chanzo cha maji cha Saibara.
VIONGOZI wakipanda miti katika chanzo cha maji cha Saibara wilayani Arumeru.
………………………….
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango amewataka wananchi wa kata ya Nkoanrua na Akeri kuheshimu mipaka uliyowekwa na bodi ya maji ya mto Pangani  katika chanzo cha maji cha chemchem ya Saibara kwa kuacha kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa chanzo hicho.
Akizindua upandaji wa miti zaifi ya 1500 katika eneo la chanzo hicho afisa mazingira wa halmashauri ya Meru Charles Mungure kwa Nina ya mkuu wa wilaya ya Arumeru mhandisi Richard Ruyango alisema kuwa  maji kutoka katika chanzo hicho yanatumiwa na vijiji vitatu vya upande wa kusini ambapo bila kuheshimu na kutunza chanzo hicho baada ya muda maji hayo yatakauka kwani kwa sasa yamepungua sana.
“Hakuna namna yoyote ambayo tunaweza kuwa na maendeleo bila kutumia maji kwahiyo nawasisiteza tena muheshimu mipaka na kutunza miti iliyooteshwa hapa leo, kwa sheria ya mazingira sheria namba 20 ya mwaka 2022 ibara ya 57 inasema umbali wa mita 60 kutoka katika chanzo cha maji na umbali huo tunaanza kuhesabu kwanzia kwenye Kingo ya chanzo sio katikati, hapatihusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu na hapa tumetumia utu badala ya mita 60 tumeweka mipaka mita 12 atakayekiuka kwanzia leo tutachukua hatua za kisheria dhidi yake,” Alisema Mungure kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru.
Sambamba na hayo pia aliagiza uongozi wa kata ya Akeri na Nkoanrua kuwatambua wananchi ambao wamepakana na na eneo hilo na kuwaandikia barua rasmi ya kuwataka kuheshimu mipaka na kuwa walinzi wa serikali kulinda miti ambayo imepandwa pamoja na kuondoa mazoa waliyoyapanda kwa muda wa siku 30 ikiwa ni pamoja na uongozi huo kutoa taarifa ya chanzo na miti iliyopandwa kila robo ya mwaka kwa mkuu wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Akeri Julius Mungure alisema kuwa  kutokana na uendelezaji wa shughuli za kibinadamu katika chanzo hicho imepelekea baadhi ya miti iliyooteshwa kwa kipindi cha mwaka jana kutoota yote huku mingine iking’olewa ambapo  kwa kuwa kumekuwa na usugu kwenye udhibiti wa eneo hilo wananchi wakabidhiwe miti hiyo waisimamie Hadi itakapokuwa ili chanzo hicho kiweze kuwa endelevu.
“Mwaka Jana tulikuja hapa tukapanda miti zaidi ya 500 lakini Leo ni michache ambayo imekuwa kwasababu wananchi wanakata Ili kufanya shughuli za kilimo hapa ikiwezekana tuweke uzio kabisa wa kuwazuia wasiweze kuingia katika eneo hili, wananchi tusiangalie leo tuu Tina miaka mingi mbele, Babu zetu na Bibi kama wasingetunza maeneo haya leo yasinge kuwepo kwahiyo niwaombe tukakitunze chanzo hiki,” Alisema Mungure
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa bodi wa bodi ya maji ya mto Pangani Felister Joseph akimwakilisha mkurugenzi wa bonde hilo Segule Segule alisema kuwa ni jukumu la bodi la maji bonde la pangani ni kutunza na kulinda vyanzo vya maji  katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, na mkoa wa Manyara(wilaya ya Simanjiro) kwa manufaa ya Sasa na vizazi vya baadae.
Alisema kuwa chanzo hicho cha Saibara ni kati ya vyanzo muhimu  ambapo matumizi ya maji ya chanzo hicho yanategemewa na wananchi wa vijiji vya Akeri, Patandi pamoja na Nduruma  kwa matumizi ya majumbani na shughuli za kilimo kwaajili ya uzalishaji na maendeleo kwa ujumla na kutokana na ongezeko la matumizi ya maji kutokana na ongezeko la watu lakini pia kwaajili ya shughuli za kiuchumi Hali hizo zinapeleka bodi hiyo kuona umuhimu wa kuendelea na jitihada mbalimbali za uhifadhi na utunzaji wa chanzo hicho.
“Ili kuweza kukinusuru chanzo hiki kutokana na uharibifu unaweza kukipelekea kupungua kwa maji na hata kukauka ndio maana wanahifadhi kwani changamoto kubwa ni shughuli za kilimo zinazofanyika ndani ya eneo la chanzo ambazo zinapeleka kupunguza ubora na kiwango cha maji,” Alisema Felista.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa eneo hilo waneahidi kushirikiana na serikali katika kuhifadhi chanzo hicho ili kiweze kuwa endelevu na kusaidia kuondoa changamoto ya maji katika maeneo mengine.

About the author

mzalendoeditor