Featured Kitaifa

MHANDISI SANGA AIPONGEZA RUWASA SONGWE KWA KUKWAMUA MIRADI CHECHEFU

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akielekeza jambo alipotembelea ujenzi wa tenki la maji katika mji wa Vwawa.

Mradi wa ujenzi wa tenki la maji litakalohudumia Kata za Uwanjani, Mwakakati, Majengo mapya na Msasani

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga (kulia) watendaji Wizara ya Maji wakimsikiliza Diwani wa Kata ya Uwanjani, Kwintin Kayombo (kushoto) walipotembelea mradi wa ujenzi wa tenki kwenye kata hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga (mwenye kofia ngumu) akikagua ujenzi wa tenki la maji Kata ya Uwanjani Wilayani unduma. 

……………………………………..

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewapongeza watendaji wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe kwa jitihada zao za kuwafikishia wananchi huduma ya maji.

Mhandisi Sanga ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na RUWASA mkoani humo.

“Nimejionea kazi kubwa na  nzuri inayofanywa na watendaji wetu wa RUWASA; Meneja wa RUWASA Mkoa wa Songwe na Mameneja wako wa Wilaya mnafanya kazi nzuri,” alisema Mhandisi Sanga.

Alisema RUWASA ilipokea miradi mingi ambayo ilikuwa haitoa maji ambapo kwa Tanzania nzima ilikuwa takriban miradi 177 na kwamba kati ya hiyo miradi karibu 30 ilikuwa kwenye Mkoa wa Songwe na sasa imekamilika isipokuwa mmoja ambao nao unatarajiwa kuanza kutoa maji hivi karibuni.

“Kama ambavyo tumekuwa tukiongea miaka ya nyuma tulikuwa na miradi mingi sana ambayo tunaita miradi chechefu takriban miradi 177 na katika mkoa huu peke yake kulikuwa na miradi chechefu karibu 30 na tunafurahi kuona miradi takriban yote imekwamuliwa katika mkoa huu wa Songwe umebaki mmoja tu nao unakaribia kukamilika,” alifafanua Mhandisi Sanga.

Alisema ukamilishwaji wa miradi hiyo ni faraja kwa Serikali kwani inakuwa imetimiza dhamira na ahadi yake ya kumtua mwanamke ndoo kichwani na aliwasisitiza kuendelea na jitihada za kuwaondolea adha wananchi.

Mhandisi Sanga alisema matarajio ya Serikali ni kuhakikisha vyanzo toshelevu vya maji vinatumika kote nchini ili kuwaondolea adha wananchi na kwamba ziara yake mkoani humo ni hatua mojawapo ya kutazama ni vipi suala hilo linafanikiwa. 

Naye Diwani wa Kata ya Uwanjani Wilaya ya Tunduma, Kwintin Kayombo akizungumza kwa niaba ya wananchi wake alipongeza jitihada za Wizara ya Maji kwa harakati zote inazoendelea nazo katika kuhakikisha wanapata huduma ya majisafi na salama.

“Kwa niaba ya wananchi hawa tumepata faraja kubwa sana baada ya kuona mradi huu wa tenki kwenye kata yetu ambao utahudumia pia na kata zingine tatu kwenye wilaya yetu; tunashuhudia mambo makubwa yakifanywa na Wizara ya Maji,” alisema Kayombo

About the author

mzalendoeditor