Featured Kitaifa

JADILINI MWONGOZO WA MPANGO WA TAIFA WA RASILIMALIWATU KWA KUTAZAMA MAENDELEO YA TAIFA KATIKA MIAKA 20 HADI 30 IJAYO

Written by mzalendoeditor

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akizungumza na wadau kutoka katika taasisi za umma (hawapo pichani) kabla ya kufungua kikao kazi cha wadau hao kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Wadau kutoka katika taasisi mbalimbali za umma wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya kufungua kikao kazi cha wadau hao kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi kufungua kikao kazi cha wadau jijini Dodoma kilicholenga kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza akiwasilisha mada kuhusu maboresho ya Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, mara baada ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi kufungua kikao kazi cha wadau kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha rasimu hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Maji, Bi. Gisela Mgomila akieleza faida ya kikao kazi cha wadau kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki kikao kazi jijini Dodoma kilicholenga kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

……………………………………

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewataka wadau wanaojadili Rasimu ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ulio katika lugha ya Kiswahili kutoa mchango utakaoliwezesha taifa kupiga hatua ya maendeleo katika kipindi cha miaka 20 hadi 30 ijayo.

Bw. Daudi ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha wadau chenye lengo la kutoa fursa kwa wadau hao kutoa mchango utakaoboresha Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma. 

Bw. Daudi amesema wadau hao wasipokuwa na maono ya muda mrefu katika kuboresha Mwongozo wa Mpango huo wa Taifa wa Rasilimaliwatu, ni wazi kuwa taifa halitapata mpango kazi mzuri wa rasilimaliwatu kwasababu mazingira ya sasa yanabadilika haraka na teknolojia inakua kwa kasi kubwa sana.

“Rasilimaliwatu ndio injini ya kila kitu hivyo, natamani uwepo wenu hapa leo ulitazame taifa litakuwa wapi miaka 20 ijayo katika maendeleo ya rasilimaliwatu, maana yake ni kwamba nyote mliopo hapa ni lazima mlitazame taifa katika miaka mingi ijayo kwani tusiporatibu vizuri suala la rasilimaliwatu ni tatizo kubwa kwa maendeleo ya taifa,” Bw. Daudi amefafanua.

Ameongeza kuwa, wadau hao wakitoa mchango utakaoboresha rasimu hiyo ya mwongozo kwa kutazama maslahi ya taifa katika miaka 20 hadi 30 ijayo watakuwa wamejitendea haki wao wenyewe, waajiri wao na taifa kwa ujumla.

Bw. Daudi amesema kikao kazi hicho muhimu kimefanyika katika wakati muafaka kwani kinatoa fursa kwa wadau kujadili Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma wa Kiswahili, ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa lakini pia ni lugha rasmi ya mawasiliano Serikalini kama ilivyo lugha ya kiingereza.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza amesema lengo la wadau hao kukutana ni kupitia na kuboresha Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili taasisi za umma ziweze kuandaa mpango kazi wenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Dkt. Rwiza amesema kuwa, kikao kazi hicho ni cha siku moja ambacho kitawawezesha wadau kupata uelewa wa pamoja na kuwapa fursa ya kutoa maoni yatakayoboresha rasimu hiyo ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma iliyotafsiriwa kwa kiswahili.

Naye, mshiriki wa kikao kazi hicho ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Maji, Bi. Gisela Mgomila amesema kuwa maoni yatakayotolewa na wadau yataisaidia Serikali na kumuwezesha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutambua mahitaji halisi ya rasilimaliwatu inayohitajika ili kutimiza lengo lake la kuwa na Utumishi wa Umma unaowajibika kwa hiari bila kushurutishwa.

Kikao kazi hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma na kimeratibiwa na Ofisi ya Rais, Menenjimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya Uendelezaji wa Ralisimaliwatu.

About the author

mzalendoeditor