Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 29 Juni 2022 akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa juu unaohusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa kuunga mkono maendeleo endelevu ya uchumi wa buluu kwa nchi zinazoendelea, nchi zinazoendelea zisizo na bahari pamoja na nchi za visiwa vidogo. Mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya viongozi wa juu ya Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake inayoendelea jijini Lisbon nchini Ureno.
******************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 29 Juni 2022 ameshiriki mkutano wa viongozi wa juu unaohusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa kuunga mkono maendeleo endelevu ya uchumi wa buluu kwa nchi zinazoendelea, nchi zinazoendelea zisizo na bahari pamoja na nchi za visiwa vidogo.
Mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya viongozi wa juu ya uhifadhi wa bahari na rasilimali zake inayoendelea jijini Lisbon nchini Ureno.
Katika mkutano huo Makamu wa Rais ametoa wito kwa mataifa kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote ikiwa ni pamoja na kuunganisha nguvu za pamoja ,kuwekeza katika teknolojia za kibunifu pamoja na tafiti.
Amesema ni muhimu kuwashirikisha moja kwa moja makundi ya kijamii ikiwemo wanawake, vijana na jamii inayotumia bahari ili kudhibiti matumizi yasiosahihi ya bahari na rasilimali zake.
Amesema ili kufikia maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu inapaswa kuzingatia hali ya kijamii, kiuchumi na kimazingira wakati wa matumizi ya rasimali za bahari kama vile ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni, kuongezeka kwa matumizi na hitaji la vyanzo vipya vya chakula, nishati na madini.
Aidha Makamu wa Rais amesema licha ya Bahari kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya Oksijeni duniani pamoja na kuwa chanzo cha ajira kwa watu zaidi ya milioni 60 na chanzo kikuu cha maisha kwa mabilioni ya watu lakini bado changamoto za uharibifu wa ikolojia ya bahari zimeendelea kuwepo ambazo zinahatarisha mfumo mkubwa wa ikolojia duniani pamoja na maisha ya watu waliowengi.
Amesema Tanzania imeendelea kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kurejesha mifumo ikolojia ya bahari , ikiwa ni pamoja na kutenga asilimia 6.5 ya sehemu ya bahari ya Hindi kuwa Maeneo Tengefu ya Bahari, kudhibiti uvuvi haramu kwa karibu asilimia 99 pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.
Makamu wa Rais amesema nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000.
Aidha ametaja eneo la maji linalochukua kilomita za mraba 64,000, hivyo kuifanya nchi kuwa tajiri kwa bionuai pamoja na uwezo mkubwa wa uchumi wa buluu ambao unasaidia, maisha ya mamilioni ya watu ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula na njia ya usafiri.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore mheshimiwa Dkt. Vivian Balakrishnan, mazungumzo yaliolenga kuongeza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili hususani katika sekta ya usafirishaji wa majini, biashara pamoja bandari.
Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu