Featured Kitaifa

MAREKEBISHO YA SHERIA ZA HABARI NA USHIRIKISHWAJI WA WANAHABARI

Written by mzalendoeditor

Na Kadama Malunde -Malunde 1 blog

Sheria kandamizi za vyombo na huduma za habari ni mojawapo ya changamoto inayokwamisha uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania. 
 
Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao ya mwaka 2015 ni miongoni mwa sheria zinazopigiwa kelele na wadau wa habari kwa kuwa chanzo cha wanahabari kukamatwa na/au kuwekwa vizuizini, vyombo vya habari kutozwa faini, na/au kufungiwa. 
 
Taasisi za MISA Tanzania na Baraza la Habari Tanzania zimekuwa mstari wa mbele kufuatilia na kuripoti ukiukwaji wa haki ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari nchini unaotokana na utekelezaji wa sheria hizi.
 
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan umetoa matumaini ya kuimarika kwa mazingira ya uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza.
 
 Hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali hii zikiwemo kufungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kuanzisha mchakato shirikishi wa marekebisho ya sheria zinazoratibu tasnia ya habari nchini.
 
Mchakato wa marekebisho ya sheria unahusisha uwakilishi wa wanahabari, wadau na Serikali ambao kwa pamoja watazipitia sheria husika, kujadiliana na kufanya marekebisho muhimu yatakayojenga mazingira wezeshi ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari, kujieleza na kupata taarifa.
 
 Katika kufanikisha hilo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Mhe. Nape Nnauye ameshakutana na makundi mbalimbali ya wanahabari wakiwemo wanahabari walio chini ya mwamvuli wa Muungano wa Watetezi wa Haki ya kupata Taarifa (CORI). Katika mkutano huo Mhe. Waziri ameelekeza iundwe timu ya wanahabari itakayofanya majadiliano na timu ya Serikali ili kupata sheria nzuri kwa ustawi wa tasnia ya habari.
 
Hata hivyo, bado kuna changamoto ya ushiriki wa wanahabari wengi kutoshiriki ipasavyo katika mchakato huu kutokana na sababu kadha wa kadha.
 
 Imebainika, kukosekana kwa mkakati mzuri wa ushirikishwaji wa wanahabari hususan walioko pembezoni (mikoani), uelewa mdogo wa sheria za tasnia ya habari na mawasiliano pamoja na vifungo korofi inachangia wanahabari wengi kujiweka pembeni. 
 
 Kuna hofu ya baadhi ya taasisi za kihabari au wanahabari wenye ushawishi kutaka kuhodhi mchakato huu au kupigania maslahi binafsi ya taasisi zao. 
 
Pia, kukosekana kwa umoja na mshikamano miongoni mwa taasisi za kihabari kunakotokana na kila mmoja kutetea maslahi binafsi.
 
Aidha, uwakilishi hafifu wa makundi kama wanahabari wanawake na wale wenye ulemavu pamoja na baadhi ya vyama/taasisi za kihabari unatishia upatikanaji wa sheria itakayolinda maslahi ya Wanahabari walio wengi. 
 
Kadhalika, uzoefu unaonesha kwamba, wanahabari wengi hawana mwamko au ari ya kushiriki katika mchakato huu na hivyo kuwaachia waandishi wachache, hususan viongoz wa taasisi za kihabari na wanahabari nguli kufanya kazi hio.
 
Hivyo, ni wajibu wa taasisi na wadau wa habari nchini Tanzania kuhamasisha ushirikishwaji wa makundi yote ya wanahabari na wadau wake katika mchakato wa mabadiliko ya sheria na sera ya vyombo vya habari.
 
 Pia, taasisi na mashirika ya kihabari yaweke utaratibu mzuri wa kukusanya maoni ya wanahabari na wadau wa habari nchi nzima pamoja na kutoa mrejesho wa mara kwa mara wa mchakato unavyoendelea. 
 
Hatua hizi zitasaidia kupanua wigo wa ushirikishwaji wa Wanahabari katika mchakato wa marekebisho ya sheria lengwa na hivyo kupelekea upatikanaji wa sheria nzuri zitakazoboresha mazingira ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari nchini Tanzania.

About the author

mzalendoeditor