Featured Kitaifa

MAENEO YALIYOTENGWA KWA AJILI YA MALISHO YA MIFUGO YATAKIWA KUSAJILIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafugaji wa Kata ya Mvua kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro ambapo amewataka wafugaji hao kuanza kulima malisho katika maeneo yao na kutunza nyanda za malisho zilizopo, vilevile kutojihusisha na migogoro ya aina yoyote katika jamii wanazoishi.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na wafugaji kupitia uongozi wao ambapo amesema zipo changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa kwenye ngazi ya Kijiji, Kata hadi Wilaya, hivyo changamoto za aina hiyo hazihitaji kuisubiri Wizara watazishughulikia wenyewe ndani ya Wilaya.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe. Innocent Kalogeris akizungumzia changamoto zilizopo kwenye jimbo lake kwa upande wa wafugaji wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro, ambapo ameshauri mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji uboreshwe ili uendane na hali ya sasa kwa kuwa wafugaji na wakulima wameongezeka.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando (kushoto) kadi ya uanachama wa Chama cha Wafugaji wakati wa mkutano wa hadhara na wafugaji uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe. Innocent Kalogeris (wa tatu kutoka kushoto) kadi ya uanachama wa Chama cha Wafugaji wakati wa mkutano wa hadhara na wafugaji uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro.

Baadhi ya wafugaji wa Kata ya Mvua wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro.

……………………..

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa maeneo yote ya malisho yaliyotengwa kwenye halmashauri yanatakiwa kusajiliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Waziri Ndaki ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara na wafugaji uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro ambapo aliwaeleza wafugaji hao kuwa halmashauri zikishatenga maeneo kwa ajili ya malisho zinatakiwa kuyawasilisha kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili yasajiliwe na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.

“Halmashauri zinatakiwa mara baada ya kutenga maeneo ya malisho katika vijiji, zinatakiwa kuyawasilisha maeneo hayo Wizarani ili yasajiliwe na kutangazwa kwenye gazeti la serikali, kwa kufanya hivyo itakuwa ni vigumu mtu kubadilisha matumizi ya maeneo hayo kwa kuwa yatakuwa yanalindwa kisheria,” alisema

Waziri Ndaki amewataka wafugaji hao kupanda malisho kwenye maeneo ambayo tayari yameshatengwa kwa ajili ya malisho badala ya kutegemea malisho ya asili peke yake. Wizara inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wafugaji kupanda malisho ili kuweza kukabiliana na tatizo la upungufu wa malisho hasa kipindi cha kiangazi.

Wafugaji wametakiwa kuacha tabia ya kuwakaribisha wafugaji kutoka maeneo mengine kuja kulisha mifugo kwenye maeneo yao kutokana na uchache wa malisho katika maeneo waliyopo. Hivyo pindi wanapowakaribisha wafugaji kutoka nje malisho katika maeneo hayo humalizika kwa haraka na kusababisha mifugo kuanza kufa kwa kukosa malisho.

Vilevile wafugaji hao wametakiwa kuanza kufanya tathmini ya kiasi cha mifugo waliyonayo na kiasi cha malisho kilichopo mpaka kuelekea msimu wa mvua kuanza. Wafugaji wametakiwa endapo wataona mifugo ni mingi kuliko malisho yaliyopo, kuanza kuvuna mifugo hiyo na kubakiza kiasi cha mifugo kitakachoendana na malicho yaliyopo badala ya kusubiri mifugo ikabiliane na kiangazi kikali ianze kufa ndipo waiuze kwa bei ya hasara kwa kuwa mifugo afya yake haitakuwa nzuri.

Waziri Ndaki pia amewaahidi wafugaji kwenye Jimbo la Morogoro Kusini kuwa Wizara itawajengea Malambo matatu na Majosho tatu, hii ni baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wafugaji zilizowasilishwa na Katibu wa Chama cha Wafugaji wakati anawasilisha taarifa yake.

Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe. Innocent Kalogeris amesema kuwa kwa sasa upo umuhimu wa kuupitia upya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji kwa kuwa lipo ongezeko kubwa la wafugaji na wakulima ili mpango huo uweze kwenda sawa na hali halisi ya sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msonda naye amesema kuwa serikali imeshafanya mambo mengi katika kutengeneza mazingira mazuri ya kuwawezesha wafugaji, kinachotakiwa sasa ni kila mmoja kuhakikisha anatimiza wajibu wake na wafugaji kufuata maelekezo / ushauri wanaopewa na wataalam.

Aidha, amesema kuwa zipo changamoto ambazo zinatakiwa kutatuliwa kwenye ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya ambazo hazihitaji ngazi ya Wizara, hivyo atawasimamia wahusika ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa kwenye ngazi hizo.

Katika ziara yake Wilayani Morogoro, Waziri Ndaki pia alifanya mkutano wa hadhara na wafugaji katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ambapo aliwasihi wafugaji hao kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa kuwa ni muhimu kwa mipango ya maendeleo ya nchi.

Pia aliendelea kuwahamasisha wafugaji kuhakikisha wanavalisha mifugo yao hereni za utambuzi zoezi ambalo linaendelea ambalo nalo lina faida kubwa katika kukuza Sekta ya Mifugo. Waziri Ndaki pia amewaahidi wafugaji wa Jimbo hilo kuwa Wizara itawajengea Majosho matatu.

About the author

mzalendoeditor