Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akifungua Mkutano wa kumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha Kanda ya Afrika kwa njia ya Mtandao unaofanyika jijini Arusha.
Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Profesa Florence Luoga akiongea na waandishi wa habari katika mkutano wa viongozi wa Benki kuu za nchi za Afrika uliofanyika mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Taifa ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nangi Moses Massawe akiongea na waandishi wa habari katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa kamati ya wanawake ya Huduma Jumuishi za kifedha Tanzania Beng’i Issa akiongea na waandishi wa habari katika mkutano huo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika wakiwa katika mkutano huo
……………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amesema mifumo jumuishi ya kifedha ya kitaifa na mpango mkuu wa maendeleo utasaidia katika kukuza matumizi ya teknolojia na ulinzi kwa watumiaji ikiwa ni pamoja kuongeza matumizi ya upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha nchini.
Dkt Mwigulu aliyasema hayo wakati Leo June 23 wakati akifungua kwa njia ya mtandao mkutano wa 10 wa mipango ya sera jumuishi ya fedha Barani Afrika uliofanyika jijini Arusha ambapo alisema kuwa sekta ya fedha ina mchango mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya uchumi nchini.
“Serikali ya Tanzania imekuwa ikichukuwa hatua za kisera katika ukuzaji wa kifedha ambapo takwimu za mwaka 2006 zimeonyesha kuwa asilimia 46 ya watu wazima waliounganishwa na huduma za kifedha ni asilimia 11 tu ya watu hao ndiyo wanaotumia huduma rasmi,” Alisema
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Florence Luoga alisema kuwa moja ya malengo ya kuanzisha huduma jumuishi za kifedha ni kuhakikisha wanawafikia wananchi popote walipo ambapo kwa Tanzania wanahakikisha kuwa mwananchi hatembei zaidi ya kilomita 15 bila kukuta huduma za kifedha ndio maana taasisi za fedha zilizopo hapa nchini zinapeleka huduma kupitia mawakala.
Profesa Luoga alisema sambamba na tasisi za kifedha pia wamehakikisha makampuni ya simu yanatoa huduma za kifedha lakini huduma hizo zitolewe kwa gharama ambayo wananchi wanaweza kumudu Ili huduma hiyo iweze kuwafikia walengwa ambao ni wale ambao walikuwa hawapati huduma za kibenki.
“katika nchi za Afrika tunaona haya yamefanyika lakini zipo changamoto ambazo sasa sisi kama viongozi tunakaa na kubadilishana mawazo kuona changamoto hizi tunazifukaje ambazo ni pamoja na athari zinazoweza kutokea katika utoaji wa huduma mtandaoni ikiwemo wizi wa utambulisho kwahiyo tumekutana kujua tutatoka na ufumbuzi gani,” Alisema Profesa Luoga.
Aidha alisema kuwa kutokana na utakatishaji wa fedha nchi za Afrika zimekuwa zikipoteza kila mwaka Dola milioni 350 ambapo kama wangechua hatua thabiti ya kuweza kuzuia ingeshuka hadi Dola milioni 10 ambapo suala hili limechukuliwa na uongozi wa ummoja wa Afrika kuangalia ni kwanamna gani kila nchi wataweza kudhibiti.
Naye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Taifa ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nangi Moses Massawe amesema katika nchi nyingi wanawake ndiyo wameonekata kuachwa nyuma katika huduma za kifedha ambapo asilimia 60 tu ya wanawake ndio wanaofikiwa na huduma za kifedha huku wanaume wakiwa ni zaidi ya asilimia 80.
Mwenyekiti wa kamati ya wanawake ya Huduma Jumuishi za kifedha Tanzania Beng’i Issa amesema kuwa karibu asilimia 10 ya wanawake wapo nyuma katika huduma jimuishi za kifedha ambapo kama kamati wamejitengenezea malengo ya kuhakikisha wanawake wanaoingia kwenye huduma jumuishi za kifedha katika nyanja zote kwanzia huduma za benki, bima na katika masoko ya hisa.
“Kwanza tutaona elimu ya fedha kwa wanawake, kuweka fedha zao kwa kutumia mifumo rasmi pamoja na mabenki kuwa na bidhaa rafiki kwao ambazo watazipenda na kuzitumia zaidi ikiwemo kupata taarifa kutoka taasisi zote za fedha zinazoenda benki kuu kujua ni wanawake wangapi wameweza kutumia bidhaa ambazo zimeanzishwa,” Alisema.