Featured Kitaifa

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE ARIDHISHWA NA MRADI WA SESSAN ENTERPRISES AWATAKA VIJANA KUENDELEA KUCHANGAMKIA FURSA 

Written by mzalendoeditor

Kiongozi wa mbio za mwenge Sahil Geraruma akiongea wakati alipotembelea mradi wa Sessan enterprises uliopo Jiji la Arusha 

Mwenyekiti wa kikundi cha Sessan enterprises Emmanuel Msafiri akisoma taarifa ya mradi wa uzalishaji wa mazao yatokanayo na mazao ya nyuki mbele ya mwenge wa uhuru.

kiongozi wa mbio za mwenge Sahil Geraruma akikagua moja ya bidhaa inayodhalishwa na kikundi cha Sessan enterprises kulia kwake ni mwenyekiti wa kikundi hicho Emmanuel Msafiri.

Baadhi ya bidhaa zitokanazo na mzao ya nyuki zinazozalishwa na kikundi cha Sessan enterprises.

……………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Kiongozi wa mbio za mwenge 2022 Sahil Geraruma ameridhishwa na mradi wa  uzalishaji wa bidhaa kwa kutumia mazao ya nyuki wa kikundi cha vijana cha Sessan enterprises  katika wilaya ya Arusha ambapo amewataka vijana kuendelea kuchangamkia fursa na sio kubaki kulalamika kuwa maisha ni magumu.
Akizindua mradi huo uliotokana na mkopo wa asilimia kumi unatolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na serikali kupitia halmashauri wenye thamani ya zaidi ya milioni 30  Geraruma alisema kuwa amezunguka karibia halmashauri 80 lakini amekuja kukutana mradi mzuri na wa kipekee  unaonyesha uhalisia wa thamani ya fedha pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana.
Alisema kuwa elimu ni kile anachobaki nacho mtu kichwani na kukifanyia kazi kama walivyofanya vijana hawa lakini niwasihi hakikisheni mnarudisha mkopo huu kwa wakati ili na wengine wakopeshwe lakini pia mkawe mabalozi waziri wa kuhamasisha vijana wengine kuja kuchua  fedha hizi na kuweza kujiajiri.
“Vijana wamefanya jambo zuri lenye manufaa kwao, kwa jamii na taifa kwa ujumla hivyo vijana wengine msikae hivyo mitaani na mkajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya badala yake jikiteni kwenye shughuli mbalimbali lakini pia halmashauri kama vikundi vimetimiza vigezo wapeni mkopo tunataka tuone mambo mazuri kama haya,” Alisema Geraruma.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi hicho Emmanuel Msafiri alisema kuwa wazo la Mradi huo  lilianza Januar, 2019  na kutekelezwa na jumla ya vijana watano ambapo lengo la mradi huo ni kukuza kipato kwa wana kikundi, kutoa ajira kwa vijana na kuongeza Pato la taifa kupitia shughuli za uongezaji wa thamani ya mazao ya nyuki nchini.
“Tunazalisha bidhaa mbalimbali za urembo, lishe na afya ambapo unatekezwa kupitia faida ya mauzo ya bidhaa zinazozalishwa pamoja na mkopo uliotokana na asilimia ya mapato ya ndani ya halmashauri na hadi sasa gharama ya mradi huu ni shilingi  milioni 36 ambayo kikundi kimechangia milioni 6 na halmashauri wakatupa mkopo wa milioni 30,” Alisema 
 Alifafanua kuwa fedha hizo wamenunulia malighafi dhana mbalimbali na mashine za uchakataji wa bidhaa ambapo wamenunua mashine tatu  lakini pia wameweza kuongeza kipato kwa kuingiza shilingi 120000 kwa siku sawa na milioni 3600000 kwa mwezi.
“Lakini pia tumetoa jumla ya ajira 10 za moja kwa moja na ajira nyingine 34 kwa vijana katika nyanja mbalimbali za uzalishaji, usambazaji wa bidhaa pamoja na kipato cha kila wanakikundi kuongezeka  na jamii wanaendelea kufurahia ubora wa bidhaa tunazozalisha,” Alisema Msafiri.

About the author

mzalendoeditor