Featured Kitaifa

BILIONI 6.8 FEDHA ZA UVIKO-19 KUTUMIKA KUNUNUA VIFAA

Written by mzalendoeditor

 

Na WyEST,MOROGORO

Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) wametakiwa kutumia kwa umahiri uwekezaji wa miundombinu na vifaa uliofanywa na Serikali katika kubuni miradi itakayotumika na wanachuo kufanya mafunzo kwa vitendo na kuzalisha ili kuongeza mapato ya Chuo.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Moshi Kabengwe wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakuu wa FDC.

Kabengwe amewataka Wakuu hao kutambua kuwa Chuo kinachotoa Elimu ya Ufundi kina nafasi kubwa ya kuwa na kiwanda kidogo cha ujuzi wa aina fulani ambacho kinakuwa ishara au kielelezo cha fani zinazotolewa na Chuo hicho.

“Wizara pia imeandaa mafunzo ikiwa ni sehemu ya kuwajenga ninyi kwenye maeneo ya uongozi na uendeshaji wa Vyuo utakaowasaidia katika matumizi ya Tehama katika kufundishia na kujifunzia, kupunguza changamoto pamoja na uanzishaji wa miradi ya kuongeza mapato,” amefafanua Kabengwe.

Aidha, Kabengwe amesema ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika Vyuo vya FDC yanatolewa kwa ubora unaokidhi soko la ajira na kuwafikia wananchi wengi zaidi, Wizara inaendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Vyuo hivyo ambao mpaka sasa umetumia zaidi ya Shilingi bilioni 33 tangu mwaka 2018.

“Kazi hii kwa sasa ipo awamu ya 3 ambayo inamalizia ukarabati wa vyuo 12 na ujenzi wa vyuo viwili. Aidha kupitia fedha za Mpango wa kupambana na Uviko 19, Shilingi bilioni 6.8 zitatumika kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo 34 kati ya vyote 54 vya umma,” ameongeza Kabengwe.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi, Bi Margaret Mussai amesema Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vinatoa mafunzo ya fani mbalimbali ya ujuzi kwa mwananchi yeyote mwenye umri kuanzia miaka 17. Ametaja fani hizo kuwa ni ufundi umeme wa magari, makenika, umeme wa majumbani, ufundi magari, useremala, ujenzi, uashi, ushonaji, upishi, kompyuta, kilimo na ufugaji.

“Kupitia jitihada zinazofanywa na Wizara, vyuo hivi vimeongeza idadi ya wanachuo kwa kiasi kikubwa kutoka 6,734 mwaka 2017 hadi kufikia 15,032 mwaka 2021. Ongezeko hili linaashiria umuhimu na uhitaji wa mafunzo yanayotolewa na vyuo hivi,” ameongeza Mussai.

Akiongea kwa niaba ya washiriki wa mkutano huo, Bi Anna Kabuje, Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania Bara ameishukuru Wizara kwa kuwezesha kufanyika mkutano huo kwani umekuwa na manufaa makubwa kwao katika kuwakutanisha pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha utendaji kazi katika vyuo wanavyosimamia.

Jumla ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 vilihamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2017 kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

About the author

mzalendoeditor