Kitaifa

NAIBU WAZIRI SAGINI ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUCHUNGUZA JUU YA UPOTEVU WA WATOTO WADOGO BUTIAMA.

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama,Jumanne Sagini ameitembela familia ya askari polisi,Konstabo Garlus Mwita aliyeuawa Loliondo na baadae kuzikwa nyumbani kwao Butiama.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,Jumanne Sagini akizungumza na familia ya marehemu Konstabo Garlus Mwita,katika Kata ya Buswahili, wilayani Butiama,

……………………………..

Na Mwandishi wetu,

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Mara kuanzisha uchunguzi juu ya upotevu wa watoto wadogo unaotokea Kata ya Buswahili, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.

Akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama amesema kuwa katika kata ya Buswahili kuna watoto wadogo watano wamepotea na mmoja kati yao amepatikana akiwa amefariki. Naibu Waziri Sagini amesema Serikali inasikitishwa na matukio hayo na kuliagiza Jeshi la Polisi mkoani Mara kufanya uchunguzi haraka ili wahalifu wapatikane na kuchukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Niwaombe Watanzania tuimarishe ulinzi na usalama wa Watoto wetu. Naliagiza Jeshi la Polisi mkoani Mara kuchunguza tukio hili na kuhakikisha wanapatikana watu au mtu au kikundi cha watu wanaohusika na upotevu wa watoto hao”

Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo leo katika kata ya Buswahili baada ya kuitembelea na kuipa pole familia ya askari Polisi, Konstebo Garlus Mwita Garlus, aliyeuawa Loliondo kwa kupigwa mshale na baadae mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Butiama mkoani Mara.

Aidha, Naibu Waziri Sagini amewahakikishia familia ya marehemu kuwa Serikali ipo pamoja nao na kwamba Jeshi la Polisi litaendela kufanya uchunguzi na kuwasaka wahalifu wa tukio hilo.

“ Tukio hili limeisikitisha sana Serikali na naomba niseme kuwa, wale wote walioshiriki katika uhalifu huo wamesakwa, watasakwa na wakipatikana lazima hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao” alisema.

Pia amewataka watu wa Butiama na wananchi kwa ujumla kuimarisha mfumo wa ulinzi shirikishi utakaosaidia kudhibiti uhalifu na kutoa taarifa za uhalifu kwenye Vyombo vya Dola.

“Uhalifu ni Mazao ya Jamii, kama jamii ikikataa uhalifu basi uhalifu hautakuwepo. Tusihifadhi watoto ambao ni wahalifu naomba tutoe taarifa kwa Vyombo vya Dola ili watoto wetu wabadilike.”

Katika hatua nyingine, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Butiama na Wawakilishi wa wananchi kwa ujumla kuimarisha usalama wa wananchi wao na kuhakikisha wanawahimiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi na wao wenyewe kushiriki katika kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyokiuka maadili ya Tanzania.

“Niwaombe wananchi kuimarisha mfumo wa ulinzi shirikishi ili tuwabaini wahalifu na kuhakikisha mnatoa taarifa kwa Vyombo vya Dola. Viongozi wa Jamii ni wawakilishi wa wananchi imarisheni usalama wa wananchi ili kudhibiti uhalifu”

About the author

mzalendoeditor