Featured Kitaifa

WATOTO WALIONJE YA MFUMO RASMI WA SHULE WAANDIKISHWA NA KURUDISHWA SHULENI

Written by mzalendoeditor

Asila Twaha, TABORA

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha watoto wote walionje ya mfumo rasmi wanaandikishwa na kurudishwa shuleni ili waweze kupata elimu ikiwa ni haki yao ya kimsingi.

Kauli hiyo imetolewa Juni 17, 2022 na Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni mgeni rasmi akimuakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa uzinduzi wa Programu ya Elimisha Mtoto.

Amesema lengo la Programu hiyo ni kuwaandikisha na kuwarudisha watoto walionje ya mfumo rasmi wa shule nchi mzima na kuitaka jamii, wazazi, walezi, watoto, wadau wa maendeo wote kwa pamoja kushirikiana na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ikiwa ni haki ya kimsingi.

Amefafanua kuwa programu hiyo pia itasadia kuweza kuwafuatilia na kujua ni kundi gani ambalo bado lipo nyuma kielimu kwa kuweza kuwafuatilia .

Balozi Batilda amesema, idadi ya watoto waliokuwa nje ya mfumo rasmi imekuwa ikipanda na kushuka na hili amesema ni kutokuwa na nguvu moja kwa jamii kuliona kuwa jambo hili ni jukumu letu sote.

Kuwepo kwa programu hiyo ambayo itaanza kwa mikoa mitatu ambayo ni Tabora, Kigoma na Songwe italeta picha ya mafanikio kwa nchi nzima na utekelezaji wa mikoa hiyo ni utekelezaji wa mikoa yote ya Tanzania.

Mhe. Batilda ametoa rai kwa watendaji wote wa elimu kuhakikisha wanafuata miongozo na taratibu katika usimamizi wa elimu ili kufikia malengo ya Serikali katika sekta ya elimu na kuwataka wazazi/walezi na jamii kuhakikisha wanasimamia suala la elimu kwa kuwaandikisha na kuwapeleka watoto shule ili kupata elimu.

“Tunaendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia suala la elimu bila malipo na pia kuliangalia suala la upatikanaji wa elimu hiyo bila ada mpaka Kidato cha Sita” amesema Mhe. Batilda

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bw. Ephraim Simbeye amesema, TAMISEMI itaendelea kufuatilia na kusimamia elimu bora kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji wa elimu.

“Natoa rai kwa watendaji wenzangu wa elimu TAMISEMI tupo nchi nzima kuanzia kijiji mpaka mtaa suala la elimu ni haki ya kila mtu watendaji wa mitaa na jamii yote tushirikiane kusimamia watoto wote wanaandikishwa na kupelekwa shuleni” amesisitiza Bw. Simbeye

Kwa upande wa mwakilishi wa UNICEF Sabrina Heavy imeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na wadau amesema, wao peke yao hawawezi kuendesha programu hiyo ila ni jukumu la pamoja kushirikiana na jamii kuendelea kupewa elimu ili kuliona suala la kupata elimu kwa watoto ni haki ya msingi.

Uzinduzi huo ulikuwa na kauli mbiu inayosema “Tushirikiana kuwaandikisha na kuwarudisha shuleni watoto walionje ya mfumo rasmi wa elimu”

About the author

mzalendoeditor