Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA ATETA NA BALOZI WA UJERUMANI NCHINI REGINE HESS

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) ameweka mkazo azma ya Wizara kuhakikisha elimu ya ufundi inatolewa kwa weledi mkubwa ili kuandaa wahitimu mahiri na wenye ujuzi.

Hayo yamejiri alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Regine Hess kujadili ushirikiano katika kuimarisha Sekta ya Elimu hususani vyuo vya ufundi nchini.

Waziri Mkenda ametoa ombi kwa Balozi huyo la kuanzisha programu ya wakufunzi wa Ufundi na Uhandisi nchini kubadilishana uzoefu na wale wa Vyuo vya Ujerumani ambapo amesema ujerumani imepiga hatua kubwa katika maeneo hayo.

Amesema ushirikiano wa Tanzania na ujerumani ni wa muda mrefu akitolea mfano kuwa ndio nchi iliyosaidia kujenga Chuo cha Ufundi Arusha na Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kupitia Taasisi ya DAAD katika miaka ya nyuma.

“Tumezungumza namna ya kuhakikisha tunaendeleza jitihada hizi kubwa zilizoanza zamani ikiwa ni pamoja na kuangalia ni kwa namna gani Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Slaam itaweza kushirikiana na ujerumani hata vyuo vikuu katika masuala ya uhandisi,”amesema Prof. Mkenda

Akizungumzia ufundishaji wa lugha ya kijerumani kama somo katika shule zetu Waziri Mkenda amesema ni suala ambalo linawezekana kwa kuwa katika mfumo wetu wa elimu zipo lugha za mataifa mengine ambazo zinafundishwa akitolea mfano Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho kinafundisha lugha nyingi ikiwemo kichina.

Kwa upande wake balozi Regine Hess ameeleza nia yao ya kuona lugha ya kijerumani ikifundishwa katika shule zetu kwa kuwa ni lugha ambayo inaweza kutumika ukizungumzia masuala ya utalii hata katika ufundi na uhandisi lengo ni kuhakikisha watoto wa kitanzania wanakuwa na elimu bora yenye ujuzi.

About the author

mzalendoeditor