Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU ACHARUKA BUNGENI UKUAJI WA UCHUMI.

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishauri serikali kuruhusu sekta binafsi iingie katika uchimbaji wa miradi ya chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma iliyopo wilayani Ludewa.

Mtaturu amesema hayo Juni 16,2022,Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/2023.

“Tumeelezwa vizuri mpango wa serikali namna utakavyokuza uchumi,lakini tumeelezwa ukuaji wa uchumi unategemea mwakani 2023,kufikia wastani wa asilimia 5.3, wakati huo Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025,inasema ukuaji wa uchumi utakuwa kwa asilimia 6.9,nikiangalia naona tumekuwa tunapanda kwa taratibu sana na sababu ni kwamba kuna baadhi ya vyanzo vya mapato hatujaviangalia,”

Amesema kumekuwa na changamoto ya kutamka lakini hatua haichukuliwi ilhali Ilani ya CCM Ibara ya 17,imeeleza wazi kutumia rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na manufaa kwa watanzia.

“Tunavyoongea leo hii kule Ludewa kuna leseni tulizowapa NDC zipatazo nane, wamezishikilia hawajahi kufanya utafiti,hawajawahi kuchimba, mali ipo ardhini haijawahi kuguswa,tulienda na Kamati yetu ya Miundombinu tumeona makaa yam awe yale huitaji kutumia nguvu kubwa,unachukua chepe unachimba unaenda kuuza,wala hayahitaji kutumia fedha nyingi leo hii kwa sababu NDC ni kampuni ya serikali hawaoni manufaa sana,ni vizuri tukaruhusu sekta binafsi ichimbe na itaenda kwa kasi kwa kuwa wao wanaangalia faida,”amesema Mtaturu.

Mtaturu amesema uwepo wa biashara hiyo ya makaa yam awe itawezesha kukuza bandari ya Mtwara ambayo itapata mzigo wa kutosha wa kwenda nje.

“Tumeanza kuona sasa hivi kuna meli zinaondoka kwenda India kutokea bandari ya Mtwara,kwa hiyo kama tutaweza kupeleka mzigo wa kutosha katika Bandari hiyo tutarudisha fedha ambazo serikali imewekeza ,niombe sana eneo hili waliangalie kwa makini ili waone namna tutakavyoongeza pato la taifa ambalo kimsingi kwetu ni jambo kubwa sana,”amefafanua.

Ili kuongeza ufanisi wa Bandari hiyo Mtaturu ameiomba serikali kujenga barabara ya Njombe -Ludewa hadi Manda yenye urefu wa kilomita 211.

Amesema kati kilomita 211 tayari serikali inajenga kilomita 50 na hivyo kuomba kilomita 161 zilizobakia nazo zijengwe ili kurahisisha usafirishaji mzigo wa makaa ya mawe na chuma kutokea Liganga na Mchuchuma.

“Kwa sababu kutakuwa na movement kubwa ya magari ambayo yatakuwa yanatoka kule kwa ajili ya kupeleka mizigo katika bandari yetu ya Mtwara na eneo lingine,ni vizuri kuifanyia kazi barabara hii ili tukuze uchumi na kuongeza pato la Taifa,”amesema.

*Pongezi kwa Rais.*

Mtaturu amempongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya na kusema ametoa kauli na kuonyesha utashi wa kweli katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Na hata hii bajeti iliyosomwa na kaka yangu Mwigulu Nchemba, imeonyesha wazi dhamira yake na imeonyesha wazi namna ambavyo anaitekeleza vizuri Ilani ya CCM,nimpongeze Waziri wa Fedha kwa kuleta hoja ambayo imeonyesha wazi inaenda kuondoa maumivu yaliyokuwepo kwa wananchi,

“Bajeti imegusa nyanja mbalimbali za kimaendeleo ,bajeti hii imegusa sekta zote kwa umakini mkubwa lakini zaidi imeonyesha wazi wazi kwamba inaenda kumgusa mwananchi mnyonge kabisa,naamini kama itaenda kufanyiwa kazi itaenda kuleta mabadiliko na kufanya mapinduzi makubwa ya uchumi wan chi yetu ,”amesisitiza.

*Serikali imeupiga mwingi Jimboni.
*
Amesema jimboni kwake ameona maendeleo mbalimbali yaliyofanywa na serikali katika sekta ya afya,maji,elimu na huduma nyingine za kijamii.

“Niishukuru serikali kwa jitihada zake, katika bajeti hii pamoja na bajeti za kisekta tulizokuwa tunapitisha nimeona katika jimbo langu wilaya yangu ya Ikungi imepata mgao wa fedha lakini kama hiyo haitoshi tumeona namna ambavyo miundombinu ya barabara itaenda kuletewa fedha kwa ajili ya kutengenezewa lami,

“Katika maeneo ya Ikungi tunapata kilomita mbili zinaenda kujengwa pamoja na taa zitawaka hii italeta mabadiliko makubwa sana,tunaishukuru kwa namna ambavyo imeamua kujenga barabara ile ya Singida kwamtoro – Kibaya -Kibrashi -Handeni ambayo tumekuwa tukiisemea kwa muda mrefu,kilomita 462 ikienda kujengwa itaenda kukuza uchumi wa wananchi wetu,tunaomba tupate mkandarasi barabara ianze kujengwa,”ameongeza.

About the author

mzalendoeditor