Featured Kitaifa

DARAJA LA TASAF LAPUNGUZA UTORO WA WANAFUNZI MJINI WINGWI

Written by mzalendoeditor

NA MWANDISHI WETU, PEMBA

WANANCHI wa vijiji vya Chupwe, Sebudawa na Mjini Wingwi wameleeza kuwa ujenzi wa daraja linalounganisha vijiji hivyo umepunguza utoro wa wanafunzi na upatikanaji wa huduma nyengine za jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika ktika shehia ya Mjini Wingi, wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba, Mwalimu dhamana wa skuli hiyo, Juma Khamis Kombo, alisema kabla ya kujengwa kwa daraja hilo, utoro wa wanafunzi ulikua mkubwa.

Alisema baada ya kukamilika kwa daraja hilo lililojengwa kupitia miradi ya jamii ulioibuliwa na wananchi wa shehia hiyo, mahudhurio ya wanafunzi yameimarika.

“Awali wanafunzi walikuwa wanashindwa kufika skuli kikawaida kutokana na kushindwa kuvuka kutoka katika makaazi yao na kwenda skuli hasa katika msimu za mvua,” alieleza mwalimu huyo.

Aliongeza kuwa awali wananchi walipanga magogo ili kuvuka kutoka eneo moja kwenda jengine kwa ajili ya shughuli za kijamii wakiwemo wanafunzi ambao walikuwa wakianguka na madaftari yao kuingia maji.

Alisema skuli hiyo yenye wanafunzi 1,272 ambapo wanafunzi watoro 118 walirejeshwa skuli kupitia mradi wa urejeshaji wa wanafunzi skuli unaoendeshwa na Wizara ya Elimu Zanzibar hapo kabla wastani wa wanafunzi 500 walikua hawahudhuri skuli kikawaida.

“Wanafunzi waliorejeshwa tulionao sasa ni wavulana 670 na wasichana 15 ambao walikuwa wakijihusisha na shughuli mbali mbali zikiwemo za uvuvi na kilimo cha mwani lakini sasa wapo skuli na baadhi yao tumewafanyia mitihani, wanaendelea vyema,” alieleza.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, waliipongeza serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) kwa kuwajengea daraja hilo lenye urefu wa zaidi ya mita 60 linalopita juu ya bwawa la maji bahari linalotenganisha vijiji hivyo.

 Aidha aliiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu kutokana na daraja hilo lililojengwa kwa miti linachakaa hivyo kuwarudisha katika dhiki waliyokuwa wakiipata awali.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Miradi ya jamii (CMC) katika shehia hiyo, Masoud Kombo Hassan, alisema awali kabla ya ujenzi wa daraja hilo kulikuwa na kikwazo kikubwa kwa wananchi hasa wanawake na watoto kuzifikia huduma zikiwemo za afya au elimu.

Alieleza kuwa hali hiyo iliwalazimu kupita katika eneo jengine ambalo ni masafa marefu kufika huduma hizo hali iliyobadilika mwaka mmoja na miezi minne baada ya TASAF kugharamia ujenzi huo na kuwataka wananchi kulitunza daraja hilo ili kutumika kwa muda mrefu.

“Tunataka tufanye harambee kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu ili kusaidia kwa kizazi cha sasa na kinachokuja kwa sababu eneo hili limezungukwa na bahari hivyo tunahitaji kivuko cha kisasa kilicho bora na cha kudumu,” alisema.

Kaimu Sheha wa shehia ya Mjini Wingwi, Hussein Makame Hamad, alisema kufunguliwa kwa daraja hilo kumerudisha furaha ya wananchi wa shehia hiyo na kusisitiza haja ya kujengwa kwa daraja la kudumu.

Aidha sheha Hamad, aliwataka watu wenye uwezo na viongozi wa jimbo hilo kusaidia ujenzi wa kudumu wa daraja hilo na ujenzi wa barabara ili kuimarisha maendeleo ya kijiji hicho.

Shilingi milioni 7.3 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo na uimarishaji wa mazingira ya eneo hilo ambapo zaidi ya miti ya mikoko 3,000 imepandwa na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini.

About the author

mzalendoeditor