Featured Kitaifa

TANZANIA YAZIKARIBISHA NCHI ZA OACPS KUADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (katikati) akimkabidhi kitabu cha kujifunza lugha ya Kiswahili Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kati na Mwenyekiti wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS Mhe. Slyvie Baipo Temon  (kushoto) akishuhudia kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia kiswahili Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede wakati wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS jijini Brussels

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (waliokaa katikati) katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022. Waliokaa kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia ni mwakilishi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi. Agnes Kiama.

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022.

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 wakiendelea na mkutano huo.

……………………………………

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amezikaribisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 7 2022.

Akitoa mwaliko huo katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, Balozi Sokoine amesema Lugha ya Kiswahili imeendelea kukua na hivyo kuwa na wazungumzaji wengi katika sehemu nyingi duniani.

Amesema Tanzania inajivunia uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni  (UNESCO) wa kuitambua na kuipa  Siku Maalum lugha ya Kiswahili hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa Tanzania.

Amesema Maadhimisho hayo yanatarajiwa kukuza zaidi na kuongeza matumizi ya lugha hiyo duniani.

“Leo hii Kiswahili sio lugha ya Taifa ya Tanzania pekee au katika nchi nyingine za Afrika bali pia ni lugha inayozungumzwa na watu wengi katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini,” alisema Balozi Sokoine. 

Ameongeza  kuwa Kiswahili sasa kinafudishwa katika zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani na ni miongoni mwa lugha za kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika.

“Kwa niaba ya Ubalozi wa Tanzania hapa Brussels na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu  tunawaalika rasmi nchi wanachama wa OACPS kuungana na Tanzania na  wadau wengine wa Kiswahili kuadhimisha kwa mara kwanza Siku ya Kiswahili duniani,” alisema Balozi Sokoine.

Tanzania na Balozi zake zitaungana na wadau wa Kiswahili duniani  kuadhimisha kwa mara ya kwanza  Siku ya Kiswahili duniani. 

Katika Mkutano huo Balozi Sokoine alipata fursa ya kukabidhi vitabu vya awali vya kujifunzia lugha ya Kiswahili vilivyoungwa na Baraza la Kiswahili Tanzania kwa Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Mhe. Slyvie Baipo Temon  na  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede.

Julai 7 ya kila mwaka ilitangazwa na UNESCO kuwa siku maalum ya Maadhimisho ya Kiswahili  duniani.

About the author

mzalendoeditor