Featured Kitaifa

MAJALIWA AWATAKA WABUNGE WAWAHAMASISHE WANANCHI WASHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI

Written by mzalendoeditor

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Semina kuhusu Sensa ya Watu na Makazi kwa Wabunge  iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni  jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa Semina  kuhusu Sensa ya Watu na Makazi  kwa Wabunge wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipofungua Semina hiyo kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni  jijini Dodoma, Mei 30,2022.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

………………………………………………….

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wabunge wawaelimishe na wawahamasishe wananchi wajitokeza na washiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na takwimu sahihi kwa makarani wa Sensa.

Akizungumza wakati alipofungua Semina ya Wabunge kuhusu Sensa ya Watu na Makazi kwenye ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma leo Mei 30, 2022, Mheshimiwa Majaliwa amesema kazi ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi inapaswa kufanywa na kila mdau wakiwemo Wabunge ambao wajibu wao ni kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu kwa wabunge kushiriki kikamilifu ili kupata taarifa na takwimu sahihi za idadi ya watu, hali zao za makazi, taarifa za majengo yote nchini hatua ambayo itawawezeshe kuwatumikia vyema wananchi.

“Tunapenda kuona kila Mheshimiwa Mbunge anaona fahari kuwa watu wote katika jimbo lake wamehesabiwa na wametoa taarifa na takwimu sahihi zinazoakisi idadi halisi ya watu na makazi yao katika eneo husika.”

Amesema Tanzania ni moja kati ya nchi chache Barani Afrika ambazo zimeweza kufanya Sensa katika vipindi vyote vya utekelezaji wa Mipango Mikakati ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa.

“Ninapenda kuwaarifu Waheshimiwa Wabunge kuwa maandalizi ya sensa yanaendelea vizuri na sasa tumefikia zaidi ya asilimia 80. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa Sensa inafanyika kama ilivyopangwa ikiwa ni pamoja na kutoa matokeo bora kulingana na viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa wakati,” alisisitiza Mheshimiwa Majaliwa .

Akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua Semina hiyo, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu amewashukuru makamisaa na watalaamu wa Sensa kwa semina na mafunzo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiwapatia wabunge kwa nyakati na makundi tofauti.

Amesema wabunge wanalichukulia suala la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi na kutoa taarifa sahihi kwa Makarani kuwa ni la msingi.

Mheshimiwa Tulia amesema Bunge litatamani kuona kwamba zoezi la sensa na Makazi ya Watu linaenda vizuri ili takwimu sahihi zitazopatikana ziwasaidie wabunge kuishauri Serikali kupanga na kugharimia shughuli za maendeleo nchini kwa kuzingatia idadi ya watu katika eneo husika.

Naye, Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu Anne Makinda amesema anashukuru kuona kwamba makundi yote waliyokutana nayo yameonesha nia na dhamira ya kutoa ushirikiano ili kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi wakiwemo Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilsihi.

Kauli mbiu ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu ni ‘Sensa kwa Maendeleo Jitokeze Kuhesabiwa’.

About the author

mzalendoeditor