Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema (Kushoto), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bw Elias Ramadhani Masumbuko (Katikati) na Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (Kulia) wakiwa wameketi kwenye moja ya madawati 100 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania ikiwa ni sehemu ya jititihaza za benki hiyo katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati mkoani humo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Afisa elimu wa Mkoa huo Bi Neema Mkanga (Kushoto) maofisa waandamizi mkoa pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema (Kushoto) akipokea msaada wa madawati 100 kutoka kwa Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (Kulia) ikiwa ni msaada kutoka benki ya Exim Tanzania katika kusaidia jitihada za mkoa huo kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Meneja wa Benki ya Exim Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa Bw Amos Lyimo (Kulia) maofisa waandamizi mkoa pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema (Kushoto) akikagua msaada wa madawati 100 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania katika kusaidia jitihada za mkoa huo kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa mwishoni mwa wiki.
Wakitoa shukrani zao kwa benki hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bw Elias Ramadhani Masumbuko (Kulia) na Afisa elimu wa Mkoa huo Bi Neema Mkanga (Kushoto) walionyesha kuridhishwa na viwango vya ubora wa madawati hayo huku wakibainisha kuwa msaada huo utasaidia zaidi kuboresha mazingira ya kufundishia kwa shule zitakazonufaika na madawati hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema (wa pili kulia) akisalimiana na Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (wa pili kushoto) wakati maofisa wa benki hiyo walipotembelea ofisi ya mkuu wa mkoa huyo ili kukabidhi msaada wa madawati 100 ikiwa ni msaada kutoka benki ya Exim Tanzania katika kusaidia jitihada za mkoa huo kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Meneja wa Benki ya Exim Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa Bw Amos Lyimo (Kushoto) na Meneja wa Benki hiyo tawi la Shinyanga Bw Japhet Mazumira
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema (katikati) Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bw Elias Ramadhani Masumbuko (wa pili kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na maofisa wa benki ya Exim walioongozwa na Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (wa tatu kulia) wakati maofisa hao wa benki hiyo walipotembelea ofisi ya mkuu wa mkoa huyo ili kukabidhi msaada wa madawati 100 ikiwa ni msaada kutoka benki ya Exim Tanzania katika kusaidia jitihada za mkoa huo kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati mwishoni mwa wiki.
………………………………..
Na Mwandishi Wetu,Shinyanga
BENKI ya Exim Tanzania imekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya Sh milioni 20 kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema ili kuunga mkono jitihada za mkoa huo katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo kero ya uhaba wa madawati. Madawati hayo yatagawanywa miongoni mwa shule zinazokabiliwa zaidi na changamoto ya uhaba wa madawati mkoani humo.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi madawati hayo iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda alisema ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo unaofahamika kama Exim Cares unayolenga kugawa madawati zaidi ya 1000 katika mikoa mbalimbali hapa nchini na ni sehemu tu jitihada ambazo benki hiyo imekuwa ikifanya kusaidia jamii inayoizunguka.
Alisema kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika kufanikisha mipango mbalimbali hususani katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini hatua aliyoilezea kuwa ndio chachu ya maendeleo kwa sekta zote ikiwemo ya benki pia.
“Msaada hu unatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 300 kwa mwaka katika kipindi cha makadilio ya miaka 10. Mkakati wetu huu wa kusaidia katika elimu unatokana na imani yetu kwamba bila kuwa na jamii iliyoelimika hata huduma za kibenki tunazozitoa lazima zitateteleka kutokana na ukweli kuwa biashara yetu hii inategemea sana mafanikio ya jamii inayotuzunguka…mafanikio ambayo tunaamini yataletwa na elimu,’’ alisema.
Alisema tangu kuanza kwa mkakati huo uliozinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa mwaka jana, tayari jumla ya madawati 500 yameshakabidhiwa katika mikoa ya Lindi, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Shinyanga.
Akizungumza mara tu baada ya kupokea msaada huo, Mkuu Mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema msaada huo umepatikana kwa wakati muafaka kwa kuwa mkoa huo unaendelea na mkakati wake wa kuboresha elimu kwa kuboresha mazingira ya masomo kwa wanafunzi.
“Katika kufanikisha hili Rais Samia Suluhu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sisi kama mkoa tunapata mahitaji yote muhimu katika elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na maslahi ya watumishi. Inapotokea wadau kama benki ya Exim wanatusaidia pia kwa msaada kama huu wa madawati wanakuwa wameunga mkono jitihada za serikali na hivyo kurahisisha ndoto za Mheshimiwa Rais ambazo ni kuboresha zaidi sekta ya elimu,’’ alisema.
Wakitoa shukrani zao kwa benki hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bw Elias Ramadhani Masumbuko na Afisa elimu wa Mkoa huo Bi Neema Mkanga walionyesha kuridhishwa na viwango vya ubora wa madawati hayo huku wakibainisha kuwa msaada huo utasaidia zaidi kuboresha mazingira ya kufundishia kwa shule zitakazonufaika na madawati hayo.
“Tunawashukuru sana benki ya Exim kwa msaada huu na tunatarajia kwamba wadau wengine wataendelea kuiga mfano huu ili kwa pamoja tusaidiane kukabiliana na changamoto hii. Kwasasa mkoa unakabiliwa na uhaba wa madawati 2500 huku jitihada za kutengeza madawati mengi zikiendelea kupitia VETA kupitia ofisi ya Mkurugenzi. Hivyo milango bado ipo wazi kwa wadau wengine kwa kuwa jitihada za pamoja ni muhimu zaidi,’’ alisema Bi Mkanga