Featured Michezo

TANZANIA NA CHINA ZASAINI MIKATABA YA SEKTA ZA UTAMADUNI NA SANAA

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mhamed Omary Mchengerwa akibadilishana  mkataba  na Balozi wa China Mheshimiwa Chen Mingjian
………………………………………..
Na John Mapepele.
Serikali ya Tanzania na China zimetiliana Saini mkataba wa makubaliano ya kusaidiana katika kuboresha maeneo ya Sekta anazozisimamia.
Utiaji wa Saini wa mikataba hiyo ya kihitoria umeongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mhamed Omary Mchengerwa kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Balozi wa China nchini Chen Mingjian kwa upande wa Serikali ya watu wa China kwenye Ofisi ya Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusiana na manufaa ya mikataba hiyo, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania imesaini mikataba hiyo ya ushirikiano inatarajia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo.
 Amesema kwa upande wa utamaduni  kutakuwa  na kupeleka wadau wa utamaduni, sanaa na michezo katika nchi ya  china na watu wa china kuja  nchini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wa elimu Tanzania itapeleka wanafunzi ambapo China itafadhili  masomo haya kwa kutoa nafasi 120 kwenda  kwenye maeneo ya lugha, utamaduni, sanaa na maeneo mengine ya hinsia (humanities) kila mwaka  ambapo Tanzania itatoa ufadhili wa nafasi 15 kwa ajili ya wachina  kuja Tanzania kusoma  hasa kwenye maeneo ya hinsia(humanities) pamoja na maeneo ya lugha.
Aidha, amesema mkataba huu unatarajiwa kutoa  nafasi kwa wataalam kwenye maeneo ya sekta hizo zote. Pia imeelezwa kuwa Serikali ya China inatarajia kujenga vituo vya kisasa vyenye miundombinu yenye viwango vya kimataifa vya sanaa na  utamaduni  ambavyo vitatumika na wasanii wa hapa nchini katika kuzalisha kazi zao zenye ubora ambazo zitauzwa duniani. 
“Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwa  wasanii wetu wanakwenda kupata studio za kisasa  kabisa  kwa ajili ya kuzalisha kazi zao”amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Aidha, amesema Tanzania inaamini kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na utamaduni uliosheheni vitu vingi kutokana na kuwa na makabila ambayo ni zaidi ya 120.
Amesema kulingana na mikataba hiyo Serikali za nchi zote zinakusudia kuchangamsha  utamaduni na sanaa ili  ziwe kwenye kiwango halisi tofauti na sasa ambapo  inaonekana  kuwa kutochangamka kwa kiwango hicho. 
Katika ziara hiyo Waziri Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi na Wakurugenzi wa Sekta za Utamaduni na Sanaa kwenye Wizara hiyo, ambapo kwa Serikali ya China Mhe. Balozi Chen Mingjian ameambatana na watendaji waandamizi kwenye sekta hizo.

About the author

mzalendoeditor