Featured Kitaifa

KANUNI MPYA YA MAFAO YA PENSHENI YATANGAZWA RASMI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni katika ukumbi wa mkutano jengo la PSSSF, Jijini Dodoma

rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya akieleza jambo katika mkutano huo.

Mkurugenzi Mtendaji, Chama cha Waajiri nchini (ATE), Bi. Suzanne Ndomba Doran, akifafanua akichangia jambo wakati wa mkutano huo na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa mkutano PSSSF, Jijini Dodoma.

…………………………………………..

Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu ametangaza rasmi kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni kufuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoelekeza mnamo tarehe 14 Mei, 2022 kuhusu mapendekezo ya kanuni ya Mafao ya wastaafu iliyoombwa na TUCTA Mei mosi, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo Mei 26, 2022 Katibu Mkuu Prof. Jamal Katundu alieleza kuwa Kanuni za mwaka 2018 zililalamikiwa na baadhi ya wadau, hivyo Serikali ilisitisha utekelezaji wake na kuelekeza Kanuni zote za mafao zilizokuwa zinatumika katika Mifuko iliyounganishwa ziendelee kutumika katika kipindi cha mpito sambamba na wadau wa utatu yaani (Serikali, Waajiri na Wafanyakazi) kukaa pamoja na kukubaliana Kanuni itakayowianisha mafao kwa wafanyakazi wote.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na imeridhia maombi ya wadau wa sekta ya Hifadhi ya Jamii ikijumuisha wawakilishi wa Wafanyakazi (TUCTA), Waajiri (ATE) na Serikali kwa kupandisha asilimia ya kikokotoo kutoka 25% iliyolalalamikiwa mwaka 2018 mpaka 33%,” alisema

Alisema kuwa Kanuni hiyo mpya ambayo imetangazwa ina manufaa mengi ikiwemo Mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF itaimarika na kuwa endelevu, kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33,  kuongeza pensheni ya mwezi kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 67 kwa waliokuwa wanachama wa PSPF na LAPF ambao ni asilimia 19 ya wanachama wote wa Mifuko ya pensheni, Mifuko itaweza kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa kuzingatia tathimini zitakazofanyika kila baada ya miaka mitatu, pamoja na Wanachama wote wanaochangia kwenye Mifuko ya pensheni watatumia kanuni moja ya mafao na hivyo kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya Wastaafu.

Alifafanua kuwa, Kanuni hiyo mpya itakuwa na vikokotoo vifuatavyo; Kiwango cha mkupuo kitakuwa cha asilimia 33 kwa Mifuko yote, Kikokotoo limbikizi kitakuwa 1/580 kama ilivyo kwa Mfuko wa NSSF na iliyokuwa Mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wanachama wa iliyokuwa PSPF na LAPF, Makadirio ya miaka 12.5 ya kuishi baada ya kustaafu kama ilivyo kwa Mfuko wa NSSF na iliyokuwa Mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wananchama wa iliyokuwa PSPF na LAPF, Mshahara wa kukokotoa mafao ya pensheni utakuwa wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu (3) ndani ya miaka 10 kabla ya kustaafu na umri wa kustaafu kwa lazima utaendelea kuwa miaka 60.

Aliongeza kuwa, pensheni za wastaafu watakaotumia kanuni hizo zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uwezo wa Mifuko ya pensheni.

Aidha, Kanuni hiyo mpya iliyoridhiwa na wadau itaanza kutumika rasmi Julai 1, 2022.

Sambamba na hayo alieleza kuwa Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa elimu kwa wananchama na umma kuhusu kanuni hiyo mpya ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa sahihi juu ya kanuni hiyo pamoja na faida zake.

Wakati huo huo, rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya amesema kuwa zoezi la uandaaji wa Kanuni mpya ya Mafao ya pensheni ilikuwa shirikishi ambapo Vyama vya Wafanyakazi, Waajiri nchini na Serikali kwa pamoja wameweza kufanikisha hayo kwa ajili ya kuhakikisha uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na wanachama kupata mafao yao.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji, Chama cha Waajiri nchini (ATE), Bi. Suzanne Ndomba Doran, alieleza kuwa Kanuni hiyo mpya ya Mafao ya Pensheni imezingatia utaalamu hivyo ameshauri elimu itolewe zaidi kwa wanachama, wafanyakazi, waajiri na wananchi ili ifahamike.

About the author

mzalendoeditor