Featured Kitaifa

JUMLA YA WALIMU 30,490 WA ELIMU YA AWALI,MSINGI WAJENGEWA UWEZO WA MAFUNZO ENDELEVU YA WALIMU KAZINI

Written by mzalendoeditor

Jumla ya walimu 30,490 wa Elimu ya Awali, msingi, MEMKWA wakiwemo walimu wa Elimu maalumu 1,889 wanatarajiwa kuwa wamejengewa uwezo kuhusu mafunzo endelevu ya walimu kazini hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.

Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakati akifungua Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwa walimu wa elimu maalum yanayofanyika Chuo cha Ualimu Patandi ambapo pia amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi chuoni hapo.

Aidha amewataka viongozi katika ngazi zote kusimamia kikamilifu mpango huo na kuweka utaratibu endelevu kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa na tija na endelevu kwa walimu.

“Serikali imeona umuhimu wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yamepelekea mifumo ya kiutendaji kubadilika pia, hivyo imeona kuna umuhimu wa kuwapa mafunzo endelevu ya walimu kazini ili kuboresha utoaji wa elimu hususan elimu maalum” amefafanua Naibu Katibu Mkuu Nombo.

Prof. Nombo amewaambia walimu hao kuwa anaamini kupitia mafunzo watakayopata yatawawezesha kwenda kufundisha walimu wengine ili kuendelea kuboresha elimu nchini.

“Nyie ni katika makundi ya mwanzo kupata mafunzo haya ambayo tunaamini mbali ya kuwasaidia kukua kitaaluma na kitaalamu bali pia yatawawezesha kwenda kutoa elimu hii kwa walimu wengine kwa ufanisi mkubwa katika maeneo mtakayopangiwa,” ameongeza Prof. Nombo.

Mratibu wa mafunzo hayo, Mwalimu Cosmas Mahenge amesema mafunzo hayo ni endelevu na yanafanyika kwa walimu wachache walioteuliwa kutoka mikoa yote ambao nao wataenda kufundisha walimu wengine nchini kote.

“Hawa walimu mnaowaona hapa ni sehemu tu, mafunzo haya yanafanyika pia katika mikoa mingine na lengo ni kuwatumia walimu hawa kuwa walimu wa wenzao kutoka pande zote za nchi,” amefafanua mwalimu Mahenge.

Naye mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo, mwalimu Omary Kingwaba akiongea kwa niaba ya washiriki wote ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kuwaletea mafunzo hayo ambayo wanaamini yataboresha kwa kiwango kikubwa ufundishaji wao.

Aidha ameiomba Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuongeza idadi ya walimu wa elimu maalumu katika shule zenye wanafunzi wa elimu maalum ili kupunguza uhaba wa walimu hao.

About the author

mzalendoeditor