Featured Kitaifa

SERIKALI YAVIONYA VIKUNDI HEWA MIKOPO YA ASILIMIA 10

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa,akizungumza  wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yaliyofanyika leo Mei 23,2022 jijini Dodoma

Katibu Mkuu, Prof. Shemdoe,akizungumza  wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yaliyofanyika leo Mei 23,2022 jijini Dodoma

SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa, wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yaliyofanyika leo Mei 23,2022 jijini Dodoma

……………………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

 SERIKALI imevionya vikundi hewa na watu wasio walengwa kwenye mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 23,2022 jijini Dodoma na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Waziri Bashungwa amesema kuwa uwapo wa mfumo huo ni njia sahihi ya kutekeleza maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu fedha hizo kutokana na hoja hiyo imekuwa ikijirudia huku kamati za Bunge zimekuwa zikitoa mapendekezo kuhusu usimamizi kila mwaka.

Waziri Bashunga amesema kuwa  baada ya kumalizika  kwa mafunzo hayo hataki kusikia vikundi hewa au fedha za mikopo zinakwenda Kwa wasiowalengwa.

“Baada ya mafunzo haya hatutaki kusikia watu wasiolengwa wanapata mikopo, baada ya mafunzo haya lazima watoke na mbinu za maarifa yaliyopatikana kwenye mafunzo tuone wanavyokwenda kufuatilia vikundi ambavyo vimepata mikopo na kuhakikishe mikopo waliyopata inakwenda kuwasaidia kubadilisha maisha yao, na sio kuwapa mikopo ilmradi tu,”amesema Bashungwa 

Aidha Waziri Bashungwa amewataka wataalamu hao kupitia sheria na kanuni za utoaji mikopo hiyo ili kuenda sambamba na mfumo huo na endapo kuna mapungufu Wizara yake itafanya marekebisho ya sheria.

Pia Bashungwa amewaagiza wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji ambayo inakusanya mapato zaidi ya Sh bilioni 5, kutenga na kutoa fedha asilimia 10 kwa ajili ya kuimarisha barabara za mitaa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Prof. Shemdoe amesema kuwa  Ofisi ya Rais-TAMISEMI imekuja na mfumo huo wa kieletroniki ikiwa  kutafuta njia bora ya kuhakikisha fedha za asilimia 10 kwa vikundi zinakusanywa, zinatumika na zinarejeshwa.

About the author

mzalendoeditor