Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU:’KILIMO CHA UMWAGILIAJI KITALETA TIJA’

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,akizungumza bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

……………………………………

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,ameomba mambo mawili katika kuboresha kilimo ikiwemo kuweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji na upatikanaji wa mbegu ya asili nchini.

Aidha,ameomba ujenzi wa mabwawa ili kusaidia wakulima wa Kata ya Kikio,Issuna ,Mang’onyi ,Misughaa na Dung’unyi kuweza kufanya kilimo cha umwagiliaji.

Mtaturu ametoa maombi hayo Mei 17,bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Amesema amefurahi katika bajeti ya mwaka huu Shilingi Bilioni 51 zimetengwa kutoka Shilingi Bilioni 17.7 zilizotengwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, ambazo zitaenda kuleta mapinduzi makubwa katika kilimo cha umwagiliaji.

“Ombi langu kama ulivyosema huko nyuma kwamba tutajitahidi kuhakikisha tume ya umwagiliaji inakwenda kwenye halmashauri zetu kule ndipo ambapo kuna mahitaji,hivyo ni vizuri likitekelezwa hili kwa kuwa wakiwa jirani wataweza kusimamia vizuri sana,”amesema.

Amesema wamekuwa na afisa kilimo ambaye anashughulika na mambo ya ugani lakini suala la umwagiliaji linaonekana kama ni la wizara ya maji hivyo ni vyema kuweka watu ambao watakuwepo muda wote wanaamka na kulala pale pale.

Ameongeza kuwa kupitia bajeti hiyo wakijipanga vizuri wanaweza kubadilisha sana kilimo cha kutegemea mvua ambacho kimeonekana kutokuwa na tija.

“Nyinyi ni mashahidi,mwaka huu tulijitahidi kupeleka mbegu na nikupongeze sana katika eneo hili tulipeleka mbegu za kutosha kama alizeti lakini mkoa wa Singida na Dodoma mvua zimekuwa chache maana yake jitihada zetu zimeenda kugonga mwamba, lakini tungekuwa na maji ya kutosha,tungekuwa na skimu za umwagiliaji za kutosha leo hii ile mbegu ambayo tumeipanda kama kule isingepotea,”ameongeza.

Amesema katika Jimbo la Singida Mashariki aliongelea skimu ya umwagiliaji ya Mang’onyi na anaishukuru wizara ilikubali kupeleka Milioni 700 ambayo itaenda kusaidia sana skimu ile iweze kuanza kazi.

“Wananchi wa Mang’onyi wanatusibiria kwa hamu lakini kama hiyo haitoshi kwenye ule mgodi wa madini ambao unaenda kufunguliwa hivi karibuni wapo tayari kununua mbogamboga kutoka kwenye mashamba ya wakulima wale ,hapa maana yake soko litakuwepo na hiyo skimu italipa ,”amesisitiza.

MBEGU.

Akizungumzia suala la mbegu ameomba kupewa kipaumbele ili ziwafikie wakulima kwa wakati na kuweza kupata tija.

“Mbegu ni roho ya kilimo, tukiwa na mbegu nzuri itasaidia kuleta mazao mengi na uzalishaji utaongezeka maana hata mnyororo wa thamani utakuwa umepatikana kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo niombe sana kuna suala ambalo tumelizungumza huko nyuma tuwe na mbegu zetu za asili na tuzilinde,

“Waziri anajua namna ambavyo GMO tumekuwa tukizitumia zaidi lakin kuna mahali ambapo tukitegemea uzalishaji wa mbegu za nje ndio tutakuja siku moja kujikuta hatuna mbegu zetu hivyo hatutakuwa salama,,na tutakuwa watumwa wa mbegu za nje,lakini tunao wenzetu wa ASA ambao ndio wakala wa mbegu nchini ,”ameongeza.

Amewashukuru viongozi wa wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya katikak uhakikisha wanamuinua mkulima.

“Mh Waziri Bashe kwenye Taifa unafanya kazi nzuri sana na unatuheshimisha ,kama kijana wa kitanzania unaonekana waziwazi wewe ni mzalendo wa kweli na hakika Rais hakukosea kukuteua na kukuweka kwenye wizara hii,hongera sana na wabunge tunakuhakikishia kuwa tutaendelea kuwaunga mkono,

“Naibu Waziri Mavunde unafanya kazi nzuri ya kumsaidia waziri na timu yenu inaonekana wazi mnaenda kufunga magoli ambayo ni ya kuboresha kilimo nchini,pongezi kwa Katibu Mkuu na watendaji wote kwa namna mlivyojipanga kukileta kilimo kiwe chenye manufaa kwa watanzania,”ametoa pongezi,

Amesema hata ongezeko la bajeti katika mwaka huu 2022/2023, ya Shilingi Bilioni 751 kutoka Shilingi Bilioni 234 ni uamuzi mkubwa na dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita katika kuwekeza kwenye kilimo nchini,nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huo na wizara kwa kupeleka mapendekezo yaliyopelekea uwepo wa ongezeko hilo.

“Tunakupongeza Waziri Bashe huu ni mwanzo mzuri, tumekuwa tukilalamika bajeti ni ndogo lakini kwa bajeti hii inaweza kuwa na nafasi nzuri yak uanzia katika kuboresha kilimo chetu,”amesema .

About the author

mzalendoeditor