Featured Kitaifa

WAZIRI PINDI CHANA ATETA NA WATAALAM WA SHERIA NA MALIKALE WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII.

Written by mzalendoeditor

   

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na watumishi wa Kitengo Cha Sheria cha Wizara hiyo ili kujadili masuala mbalimbali yanayo husu Sheria zinazosimamia shughuli za Uhifadhi wa Maliasili, Malikale na uendelezaji Utalii hapa nchini.

Akizungumza na watumishi hao leo jijini Dodoma, Waziri Chana amewataka  wafuatilie kwa karibu masuala yote ya kisheria yanayoihusu Wizara  ya Maliasili na Utalii na kuhakikisha wanaiepusha Wizara na migogoro inayoweza kuepukika.

Katika hatua nyingine Waziri Chana amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi na watumishi wa Idara ya Mambo ya Kale  pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo kuhusu uendelezaji wa rasilimali za Malikale.

Licha ya kazi nzuri inayofanywa na Idara hiyo, Mhe. Chana ameitaka Idara hiyo iendelee kuboresha maeneo ya Malikale nchini ili yavutie watalii wengi zaidi.

Aidha, ameitaka Idara hiyo iwe na mkakati wa kutambua maeneo mapya yanayo stahili kuingizwa kwenye orodha ya Malikale kwenye mikoa mipya.

Mhe. Chana ameongeza kuwa Idara hiyo inapaswa kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watalii wanaotembelea maeneo ya vivutio vya Malikale pamoja na kuonesha  mchango wake katika uchumi wa nchi.

Awali akiwasilisha taarifa ya Utendaji kazi wa Idara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt. Kristowaja Ntandu ameeleza kuwa pamoja  na  kuvutia watalii, sekta ya Malikale nchini  inachangia kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na kutengeneza nafasi za ajira kwa wananchi walio katika maeneo yenye malikale hizo.

About the author

mzalendoeditor