Burudani Featured

FAMARA ENTERTAINMENT NA UVCCM MWANZA KUFANYA KAZI ZA PAMOJA KUINUA WASANII NA WACHEZAJI

Written by mzalendoeditor

KATIKA kuhakikisha Sanaa na Utamaduni wa Mkoa Mwanza inakua kwa kishindo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Famara Entertainment Fabian Fanuel amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo ya kina ya jinsi ya kuweza kuinua Sanaa na Utamaduni Mkoani hapo.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ofisi ya UVCCM Mkoa wa Mwanza, Katibu Mkuu wa UVCCM Mkoa wa Mwanza Dennis Kankono ameipongeza Famara Entertainment kwa jinsi inavyopambana kuwaunganisha wasanii wa mkoa wa Mwanza kuwa na Umoja na ushirikiano ili kuweza kuviendeleza vipaji vyao vifike hatua nzuri zaidi.

Bwana Kankono amemshukuru Mtendaji Mkuu wa Famara Entertainment kwa kuendelea kupambania sanaa, utamaduni na Michezo katika Mkoa wa Mwanza kwa nguvu kubwa na matokeo yake yanaonekana pamoja na kuwepo changamoto kadhaa wa kadhaa.

Amesema UVCCM itaendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Taasisi ya Famara Entertainment kuhakikisha wanafikia lengo la kuweza kuwapeleka wasanii, wanamuziki na wanamichezo hatua kubwa katika kuona faida za vipaji walivyonavyo.

“Kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya kama taasisi, najua mnatumia muda wenu mwingi kuhakikisha vipaji vya vijana wa Mwanza vinakua na kuleta matokeo chanya katika maisha yao, kwa niaba ya Umoja wa vijana tunawapongeza sana”.

“Yapo mambo mengi huko mbele tunahitaji kufanya pamoja ili kuendeleza vipaji vya hawa vijana wetu, na ninaamini kwa ushirikiano wenu Famara Entertainment na sisi UVCCM tutafanya mambo makubwa huko mbele, zaidi tuendeleee kushirikiana kwa mambo mbalimbali” alisema Dennis Kankono.

Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Famara Entertainment Bwana Fabian Fanuel amemshukuru Katibu Mkuu wa UVCCM Mkoa wa Mwanza Dennis Kankono kwa kazi kubwa yanayofanya katika kuendeleza mambo ya vijana pamoja na vipaji walivyonavyo.

“Tumeona mambo mengi mmeyafanya kwa vijana hapa Mwanza, mengine katika Sekta ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, tunawaomba muendelee kuwakumbuka na kuwapa fursa na nafasi za kutosha vijana wote wa Mwanza wenye vipaji vya aina mbalimbali ili waweze kuonyesha walivyonavyo” alisema Fabian Fanuel.

Aidha Fanuel amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoingoza kwa kuweka mazingira mazuri kwa wasanii katika kuwapa nafasi baadhi yao kuonyesha sanaa zao na hasa na utoaji wa Mirabaha waliyopewa wasanii hivi karibuni.

About the author

mzalendoeditor