Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akifungua kikao cha Kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa, kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akieleza jambo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa kilichofanyika jijini Dodoma .
Mwenyekiti wa Kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa Angellah Kairuki akieleza lengo la kamati hiyo katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11/05/2022.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, akishiriki kikao cha Kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11/05/2022.
Wajumbe wa Kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa wakiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11/05/2022.
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula pamoja na wajumbe wa Kamati ya ushauri na uratibu wa utekelezaji wa ahadi za nchi katika Jukwaa la kizazi chenye usawa baada ya ufunguzi wa kikao cha Kamati hiyo kupokea na kujadili mpango kazi wa utekelezaji wa ahadi hizo kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Mei, 2022
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (WMJJWM)
***************************
Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amewataka Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa kukamilisha Maazimio ya Beijing ya miaka 27, tangu Beijing iweke maazimio ya kuwa na kizazi chenye Usawa kwani ndio matamanio ya Mhe. Rais Samia.
Aidha amewata Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kitaifa ya kushauri na kuratibu utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa kufanya kazi kwa weledi na kuwa chachu ya mabadiliko kuelekea kizazi chenye usawa.
Dkt. Gwajima ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati hiyo chenye lenyo la kupokea rasimu ya mpango kazi wa utekelezaji wa ahadi hizo, kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11/05/2022.
Mhe. Dkt. Gwajima amesema Kamati ikifanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha ahadi za nchi zinatekelezwa katika Jukwaa, utakuwa ni mwanzo wa kizazi chenye usawa na kuwa nchi ya mfano wa kuigwa.
“Mhe. Rais amedhamiria kuhakikisha nchi inakwenda sambamba na ulimwengu na haimwachi mtu nyuma kwa visingizio vyovyote hasa wanawake walioachwa nyuma kwa miaka mingi ambako kumesababisha maendeleo duni kwa watoto wa kiume na wa kike, hivyo tunapaswa kuhakikisha mlolongo huo tunaumaliza ili jamii yote tuwe na kizazi cheye usawa na kuongeza kasi ya maendeleo maradufu” alisisitiza Mhe. Gwajima.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula akizungumza katika kikao hicho amebainisha kwamba, Kamati hiyo tangu iteuliwe imekuwa na ushirikiano mkubwa na Wizara katika kuhakikisha matarajio ya nchi yanafikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Angellah Kairuki ameishukuru Wizara kwa ushirikiano katika kufanikisha kuwa na rasimu ya mpango kazi utakaotumiwa na Kamati hiyo kufanya kazi yake ya kuratibu ahadi za nchi kufikia kizazi chenye usawa.
“Malengo yetu ni kuwa na mpango mkakati unaokidhi mazingira ya nchi yetu na usiomwacha mtu nyuma, tangu Desemba mwaka jana Kamati imeshafanya vikao vinne kwa ajili ya kupitia rasimu ya mpango kazi huu na sasa tupo tayari kupokea” alisema Kairuki.
Kairuki ameongeza kuwa hatua zinazofuata ni kuwa na vikao kwa upande wa bara na Zanzibar ambapo Kamati itakutana na wadau wa mbalimbali kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi, vingozi wa Dini, Makundi maalum, Wasanii, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, TUCTA, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, ZATUC, Vijana na na vituo vya ubunifu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliiteua Kamati hiyo ya Kitaifa mnamo tarehe 16 Desemba, 2021 kwa lengo la kushauri na kuratibu utekelezaji wa ahadi za nchi katika Jukwaa la kizazi chenye usawa, ambapo Mhe.Rais alichagua kutekeleza eneo la pili la kuhakikisha usawa wa jinsia.
Mpango kazi huo unaoandaliwa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu ili Kamati hiyo ianze kuufanyia kazi.