Featured Kitaifa

WAZIRI MAKAMBA AWAHAKIKISHIA SOKO LA NDANI WADAU WA NGUZO ZA UMEME ZA MITI NCHINI

Written by mzalendoeditor


Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Wadau wa nguzo za miti( hawapo pichani), kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga, katika mkutano wake na wadau hao uliofanyika, Mafinga mkoani Iringa, Aprili 30, 2022.

Baadhi ya Wadau wa Nguzo wakimsikiliza Waziri wa Nishati, January Makamba( hayupo pichani), wakati wa Mkutano wa Waziri huyo na wadau hao kuhusu uzalishaji wa nguzo bora uliofanyika, Mafinga mkoani Iringa, Aprili 30, 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said,akizungumza na Wadau wa nguzo( hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Wadau hao kuhusu uzalishaji wa nguzo bora uliofanyika, Mafinga mkoani Iringa, Aprili 30, 2022.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Maharagwe Change,akizungumza na Wadau wa nguzo( hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Wadau hao kuhusu uzalishaji wa nguzo bora uliofanyika, Mafinga mkoani Iringa, Aprili 30, 2022.

********************************

Ø Aunda Kamati maalum itakayowezesha upatikanaji wa nguzo zenye ubora zaidi

Na Zuena Msuya, Iringa

Waziri wa Nishati, January Makamba amewatoa hofu wadau wa nguzo za Miti za Umeme nchini kwa kuwahakikishia soko la kuuza nguzo zenye ubora kwa Shirika la Umeme nchini( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), hapa nchini.

Aidha, amewataka Wadau hao kuzalisha nguzo hizo zenye ubora ili Serikali iweze kuwatafutia masoko ya nje kwa kuwa wana uwezo kuzalisha zaidi kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya sasa na ziada.

Makamba alisema hayo wakati wa mkutano wake uliohusiha Wazalishaji, Wasafirishaji, na Watengenezaji wa nguzo za miti za Umeme, kutoka Mkoa wa Iringa na Njombe, uliofanyika Mafinga Mkoani Iringa, Aprili 30, 2022.

Mkutano huo umelenga kuondoa sintofahamu pamoja na minong’ono inayoendelea kwa baadhi ya watu wanaopotosha kuwa Serikali haitanunua nguzo za Umeme za ndani na badala yake zitaagizwa kutoka nje ya Nchi.

Katika mazungumzo yake na Wadau hao, Makamba alisema kuwa, Serikali itaendelea kununua nguzo za miti za Umeme kutoka kwa wazalishaji wake wa ndani ili kulinda viwanda vya ndani kwa kuzingatia ubora wa nguzo uliowekwa.

“Lengo la Serikali ni kukuza uchumi wa wananchi wake kwa kuboresha bidhaa zao kwa kuwasimamia katika kuzalisha kwa vigezo na ubora uliowekwa, ili wananchi hao waweze kunufaika na kukuza uchumi wao na pato la Taifa kwa ujumla”, Alisema Makamba.

Pamoja na Mambo mengine, aliwataka Wadau hao kuhakikisha wanazalisha nguzo zinazokidhi viwango na ubora unaotakiwa kimataifa ili kuweza kukidhi soko la ndani na hata nje ya Nchi kwa kuwa mikoa hiyo inaongoza kwa kuwa na uzalishaji wa nguzo.

Alisema kuwa, Serikali itakikisha kuwa biashara ya nguzo za miti za Umeme, inakuwa zaidi Kitaifa na kimataifa kama Nchi zingine zinavyofanya ikiwemo Afrika Kusini ambao wanauza nguzo kama hizo katika nchi nyingine.

Kwa Mantiki hiyo, ameelekeza kuundwa kwa Kamati ya watu 12 kutoka katika kila kundi la Wadau wa nguzo za miti za Umeme, katika Mikoa ya Njombe na Iringa, Wizara na Taasisi zake pamoja na Shirika la Viwango nchini ( TBS) ili kuongeza ufanisi katika kuzalisha nguzo zenye ubora unaolidhi viwango.

Kamati hiyo pia itatoa ushauri sahihi kwa Wadau hao juu ya njia bora za kufuata na kuzingatia ili kupata bidhaa zilizobora zitakazo kubalika Kitaifa na kimataifa.

Waziri Makamba amewataka Wadau hao kuunda chama Cha wazalishaji wa nguzo ili kiweze kudhibiti ubora unaotakiwa na hata kutoa adhabu kali kwa atakayebainika kuzalisha chini ya Kiwango pamoja na kuandaa sheria zitakazoongoza chama hicho.

Aidha ameutaka umoja huo kwenda kujifunza zaidi, namna ya kudhibiti ubora wa nguzo kwa nchi zilizofanikiwa ikiwemo Afrika Kusini ili kuleta ushindani zaidi.

“Ni vyema mkawa na Cha ma chenu kinachotambulika kisheria, Cha hiki ni chombo muhimu katika kuwasimamia na kuwaongoza, vilevile kitakuwa kinatumika kudhibiti ubora wa nguzo zinazozalishwa kwani atakayekuwa akienda tofauti mtamshungulikia na hata kumpatia adhabu pale atakapokuwa akienda kinyume na kuharibu soko”, Alisisitiza Makamba.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Maharagwe Change, aliwataka Wadau hao kuwa waaminifu pale nguzo zao zinapotakiwa kupelekwa katika maeneo ya miradi kwa kuweka nguzo halisi zilizokaguliwa na siyo kufanya udanganyifu wa kuweka zisizokuwa na ubora.

Amesema kumekuwa na changamoto ya nguzo kuharibika baada ya muda mfupi kutumika kutokana na kuwa chini ya kiwango na ubora unaotakiwa, huku nguzo hizo zikiwa tayari zimekaguliwa na kuonekana zina ubora unaotakiwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amewahakikishia Wadau hao kuwa soko la nguzo lipo la kutosha kwani bado miradi mingi ya usambazaji wa Umeme vijijini inaendelea na nguzo nyingi zinahitajika.

Akitoa mfano Mkoa wa Iringa kuwa kuna Mradi wa Ujazilizi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni katika Mkoa huo na mikoa mingine.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, alimuhakikishia Waziri wa Nishati kuwa atashirikia na Wadau hao kutekeleza yake yanayotakiwa ili kupata bidhaa Bora na hatimae Mikoa hiyo iwe kinara katika kuzalisha nguzo na bidhaa za miti zenye ubora unaotakiwa.

Amewataka Wadau hao kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika na kuwa wasikivu kwa kile watakachokuwa wakielezwa kwa lengo la kupata bidhaa Bora kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.

About the author

mzalendoeditor