Na WAF – Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo ameagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Tigest Ketsela Mengestu aliyemaliza muda wake kutumikia nafasi hiyo hapa nchini.
Dkt. Tigest ambaye amedumu katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka minne hapa nchini ameagwa rasmi na Waziri Ummy Mwalimu pamoja na Menejimenti ya Wizara katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Waziri Ummy ameishukuru WHO kwa kuendelea kuwa karibu na Serikali na kutoa ushauri wa kitaalam, maoni na msaada kwenye masuala mbalimbali ya kupambana na magonjwa ambukizi na yasiyoambukiza.
“Mchango wa WHO katika kipindi chako hapa nchini unaonekana wazi, mmeweza kutusaidia Serikali kuboresha sekta ya afya na utekelezaji wa afua mbali mbalimbali za mapambano dhidi ya magonjwa” amesifu Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi na WHO pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa inaboresha mifumo ya afya na Sekta ya afya kwa ujumla ili kujengea uwezo nchi na wataalam wetu kutambua na kudhibiti magonjwa
Kwa upande wake Dkt. Tigest ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya nchini na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mashirika ya kimataifa ikiwemo WHO kufanya kazi nchini.
“Ninashukuru sana kwa ushirikiano wenu mliotoa kwangu na kwa WHO, Mwenyezi Mungu awabariki wote na nashukuru sana kunipa nafasi ya kufanya kazi na Tanzania” ameshukuru Dkt. Tigest.