NA MWANDISHI WETU, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kuiendeleza na kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa maslahi ya Wazanzibari wote.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na Mwenyekiti mpya wa Chama Cha ACT – Wazalendo Juma Duni Haji ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha rasmin.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ujio wa kujitambulisha pamoja na kufanya mazungumzo na kiongozi huyo ni mwelekeo mzuri wa kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na mustakbali mpana wa kuiiendeleza Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti huyo mpya wa ACT- Wazalendo Taifa kwa kuchaguliwa na chama chake kushika wadhifa huo.
Nae Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa Juma Duni Haji kwa upande wake alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kupata fursa ya kuja kujitambulisha kwa Rais pamoja na kujadili masuala mbali mbali juu ya mustakbali wa Zanzibar.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alieleza kuwa mbali ya mazungumzo hayo pia, amepokea wito wa Rais Dk. Mwinyi wa kutaka kukaa pamoja na kujadili masuala yenye mustakbali wa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi mara nyingi amekuwa akisisitiza umuhimu wa kukaa pamoja na kuzungumza badala ya kubishana kwenye majukwaa na kutupiana maneno.
Hivyo, alieleza jinsi alivyovutiwa na wito huo wa Rais Dk. Mwinyi ambao una umuhimu mkubwa juu ya mustakbali wa Zanzibar.
Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alitumia fusra hiyo kumpongza Rais Dk. Mwinyi kutokana na ukaribisho wake sanjari na mazungumzo yao ambayo yalikuwa mazuri huku akiahidi kuwaeleza wanachama wake juu ya suala zima la maridhiano linavyoendelezwa kama vile ilivyokusudiwa.
“Mimi Mwenyekiti wao nimehakikishiwa na Mheshimiwa Rais kwamba hakuna tatizo ya yale yote waliyokubaliana na Marehemu Maalim Seif kwani sote tuna nia ya kuijenga nchi yetu”, alisema Mwenyekiti huyo mpya wa ACT- Wazalendo.
Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alitumia fursa hiyo kuwanasihi wanachama wa chama hicho kuendeleza siasa zenye tija na kuepuka vijembe majukwani kwani hatua zilizokusudiwa katika kuiendeleza Zanzibar zinakwenda vizuri.
Juma Duni Haji alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha ACT- Wazalendo Taifa kufuatia uchaguzi uliofanyika kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho mnamo Januari 29, 2022