SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson ametangaza kifo cha Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 24,2022 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge jijini Dodoma imeeleza kuwa, Mheshimiwa Ndyamkama amefariki leo Aprili 24,2022 katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani wakati akipatiwa matibabu.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama, Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, waheshimiwa wabunge na wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Mwenyenzi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,”amesema Mheshimiwa Spika.
Aidha, Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.