Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde amemshukia Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na watu wanaomsema vibaya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli na kumsema vizuri Rais Samia Suluhu Hassan ni wanafiki kwa sababu watamgeuka Rais Samia pindi atakapoondoka madarakani.
Kauli ya Lusinde imekuja baada ya hivi karibuni Zitto alikaririwa kwenye mitandao ya kijamii akiwakosoa wanaomsifia Hayati Rais Magufuli.
Lusinde ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 22, 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi ya Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2022/2023, ambapo amesema licha ya ushirikiano uliopo kati ya vyama vya CCM na ACT Wazalendo visiwani Zanzibar, ameshangazwa na Zitto kumnanga Hayati Magufuli kana kwamba Zitto hashiriki katika Serikali ya Zanzibar.
“Nataka niseme Marehemu Magufuli aheshimiwe, kufiwa ni suala kubwa haiwezekani kulizungumza kwenye utawala bora suala la Magufuli kusemwa vibaya na mimi sitaacha.
“Zitto anatutaka tunaompenda Magufuli tukazikwe naye. Zitto amewahi kufiwa na mama yake mimi sitaki kuingia huko mama wa Zitto ni mama yangu mimi ametanguliwa. Mimi nimewahi kufiwa na baba yangu lakini ACT Wazalendo wamewahi kufiwa na Maalim Seif wanataka tumseme vibaya sisi hatuwezi,”amesema.