Featured Kitaifa

WIZARA YA MADINI ITAENDELEA KUWASIKILIZA WADAU WAKE

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza na Viongozi wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMATA) alipokutana nao katika Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMATA) Bw. Jeremia Kituyo akiwasilisha taarifa na changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta ndogo ya biashara ya madini kwa Waziri wa Madini Dkt. Biteko walipokutana naye katika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma.

Viongozi wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMATA) wakimsikiliza Dkt. Doto Biteko wakati akizungumza katika kikao

Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko na Viongozi wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMATA) alipokutana nao mara baada ya kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma.

………………………………………..

WAZIRI wa Madini, Dkt.Doto Biteko amesema, wizara yake itaendelea kuwasikiliza wadau wote wa Sekta ya Madini ili kuzungumza kwa pamoja kuhusu shughuli za madini

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMATA) alipokutana nao kuzungumza kuhusu ukuaji na usimamizi wa sekta ndogo ya biashara ya madini katika Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma.

Dkt.Biteko amesema kuwa, Wizara ya Madini imekuwa ikikutana na wadau wote wa Sekta ya Madini kupitia maonesho mbalimbali ya madini na mikutano inayofanyika hapa nchini ili kuwasikiliza na kuzungumza nao kuhusu changamoto mbalimbali za sekta na kuzitafutia majawabu.

Ameongeza kuwa, wizara inatarajia kuendelea kukutana na makundi maalum mbalimbali ili kuwasikiliza na kutatua changamoto kwa pamoja na kuwataka CHAMATA washikamane katika umoja wao Ili kuwa na sauti ya pamoja kama ilivyo kwa vyama vingine vilivyopo katika Sekta ya Madini.

Dkt. Biteko amewataka CHAMATA kuimarisha umoja wao na kuhakikisha wanakisajili chama chao ili kiwe chama imara kabla hawajapeleka malalamiko yao kwa Serikali.

“Nimefurahi mno, hamna mtu aliyewashawishi kuunda chama, nyie wenyewe mmeamua kuunda hicho chama, nendeni mkakisimamie vizuri, “amesema Dkt.Biteko.

Akizunguzia kuhusu utoroshaji wa madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu, Dkt.Biteko amewataka CHAMATA kuwa mabalozi kwa wafanyabiashara wenzao katika kuhamasisha kuacha kutorosha madini.

Amesema, Serikali imeweka Masoko ya Madini ili kuondoa urasimu na kuongeza kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Mwanza aliagiza watu wapeleke madini yao kwenye masoko kutoka sehemu yoyote na wauze bila kusumbuliwa.

“Ninataka kutumia nafasi hii kuwaomba wale wote tuliopewa dhamana ya kusimamia Sekta ya Madini, wale watu ambao wanapeleka madini sokoni wasisumbuliwe, mtu asipate msukosuko, aone raha ya kwenda sokoni, soko liwe mahali pa kimbilio la wachimbaji, “amesisitiza Dkt. Biteko.

Naye, Mwenyekiti wa CHAMATA, Bw. Jeremia Kituyo amesema kuwa, CHAMATA inataka kuona Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa ili Tanzania inufaike ipasavyo na rasilimali ya madini nchini.

Aidha, Kituyo ameishukuru wizara kwa uanzishwaji wa Masoko ya Madini nchini ambayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa wafanyabiashara wa madini.

kikao hicho, kilihudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka Tume ya Madini na Wizara ya Madini ikiwa ni mwendelezo wa Waziri wa Madini kukutana na kuzungumza na wadau mbalimbali kuhusu Sekta ya Madini.

About the author

mzalendoeditor