Uncategorized

WAZIRI NAPE:’ANWANI ZA MAKAZI KUTUNZA HISTORIA YA NCHI’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiwa na Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara yake katika mkoa huo kukagua utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akikagua kibao chenye anwani ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mjini katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma. Aliyeambatana naye ni Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akisimika nguzo yenye jina la barabara ya Chikongola mkoani Mtwara. Kushoto ni Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akibandika jina la barabara ya Chikongola kwenye nguzo kabla ya kuisimika katika moja ya barabara za mkoa wa Mtwara.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akisimika nguzo yenye jina la barabara ya Uhuru katika mkoa wa Lindi.

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza akizungumza na baadhi ya watendaji wa Mkoa wa Lindi (hawapo pichani), wakati wa ziara ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye (kulia) katika mkoa hio kukagua utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi

………………………………………………….

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa rai kwa wananchi na viongozi wa mikoa na halmashauri kuweka majina ya barabara na mitaa ambayo yatalinda historia ya nchi

Rai hiyo ameitoa leo tarehe 13 Aprili, 2022 wakati wa ziara yake katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi kukagua na kuhamasisha kasi ya utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi

Amesema kuwa, “Zoezi hili litumike kulinda historia ya nchi yetu, tusiache ikapotea tutumie majina ya viongozi mashuhuri pamoja na watu mashuhuri ili watoto wetu na vizazi vijavyo watakaokuja kutumia mfumo huu wakiuliza kwanini jina fulani basi wapatiwe historia ya jina husika “.

Ameongeza kuwa upo mwongozo mdogo wa uundaji wa majina ya barabara, mitaa na njia unaoruhusu wananchi kukubaliana na kuchagua jina la barabara na mtaa lakini sio vibaya katika baadhi ya maeneo wakitumia majina ya viongozi mashuhuri na watu mashuhuri ili kulinda historia ya nchi

Katika hatua nyingine, Waziri Nape amezielekeza sekretarieti za mikoa kuandaa mifumo madhubuti ya kulinda miundombinu ya Anwani za Makazi dhidi ya uharibifu unaoweza kufanywa na watu wasiothamini maendeleo ya nchi

“Tuweke mifumo ya kulinda miundombinu ya mfumo huu, kwasababu kuna watu wanaweza kuiharibu kwa makusudi kwa kuitoa na kwenda kuiuza chuma chakavu, hivyo tuandae mifumo madhubuti ya kuilinda na kuwashughulikia waharibifu wa miundombinu hii”, amesisitiza Waziri huyo

Aidha, Waziri Nape ameridhishwa na utekelezaji wa mfumo huo katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ikiwa ni mikoa iliyopo katika kumi bora kwenye utekelezaji wa Operesheni hiyo kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana katika mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi

“Sio kwamba hatuziamini sekretarieti za mikoa katika kutekeleza operesheni hii, ukweli ni kuwa mnafanya kazi nzuri lakini Wizara ninayoisimamia ina wajibu wa kufika na kukagua namna utekelezaji wa operesheni hii unavyoendelea na vibao vinavyowekwa ili ifikapo mei 22 mwaka huu wa 2022 tuukabidhi mfumo ukiwa salama, kamili na tayari kutumika”, amesisitiza Waziri Nape

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema utekelezaji wa operesheni hiyo katika mkoa wake umefikia asilimia 97 na katika mkoa huo zoezi linakwenda vizuri na litakamilika kabla ya tarehe 30 Aprili mwaka huu

Kwa upande wa Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amesema utambuzi umekwishakamilika kwa asilimia 100, zoezi lililobaki ni kuingiza taarifa kwenye mfumo wa kidijitali na kusimika nguzo za majina ya barabara na mitaa na kabla ya tarehe 30 mwezi huu wa Aprili zoezi litakuwa limekamilika

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza ametolea ufafanuzi kwa maeneo ambayo yamepimwa lakini bado hayajaendelezwa kuwa ni lazima yatapewa namba na taarifa zake zitaingizwa kwenye mfumo

“Msingi wa anwani yeyote ni kiwanja hata kama hakijajengwa taarifa zake ni lazima ziingizwe kwenye mfumo wa utambuzi wa kidijitali wa Anwani za Makazi ili hapo baadae patakapoendelezwa mfumo wa utaonesha nyumba hiyo au jengo hilo ni namba ngapi”, amesisitiza Mhandisi Ichwekeleza

About the author

mzalendoeditor