Na Zuena Msuya, Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema utekelezaji wa miradi ya kufua umeme kwa kutumia nguvu ya upepo katika Mkoa wa Singida inatarajiwa kukamilika kati ya mwaka 2023 na 2027.
Miradi hiyo inatekelezwa na wawekezaji binafsi wenye nia ya kuzalisha umeme na kuliuzia Shirika la Umeme (TANESCO).
Wakili Byabato alisema hayo wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Bungeni Jijini Dodoma, Aprili 13, 2022, akijibu swali la Mhe. Jesca Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kufahamu utekelezaji wa mradi huo mkoni Singida.
Katika majibu yake, Naibu wa Waziri wa Nishati alieleza kuwa miongoni mwa miradi hiyo, ni Mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 50 kwa kutumia nguvu ya upepo, utakaotekelezwa na Kampuni ya Upepo Energy, katika eneo la Msikii, Halmashauri ya Singida Vijijini.
Majadiliano ya mkataba wa kuuziana umeme (Power Purchase Agreement), kati yake na TANESCO yanaendelea.
Wakili Byabato alisema kuwa mradi mwingine wa Megawati 300 utakaotekelezwa na Kampuni ya GEO Wind ambao unahusu ujenzi wa mitambo ya kufua umeme katika eneo la Kititimo, Halmashauri ya Singida mjini.
Majadiliano baina ya mwekezaji na mfadhili Green Climate Fund (GCF) yanaendelea.
Pia, amesema Mradi mwingine wa tatu ni wa ubia kati ya Shirika la Umeme (TANESCO) na Kampuni ya Abu-Dhabi (Masdar) utazalisha Megawati 100, katika eneo la Ikungi, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.